Mbinu ya kuepuka vifo vya magonjwa ya dharura, ajali yatajwa

Muktasari:

  • Wataalamu bingwa waliosomea fani hiyo nchini ni 27 pekee huku wengine tisa wakitarajiwa kuhitimu masomo yao mwaka huu.

Imeelezwa kuwa asilimia 40 ya vifo vitokanavyo na kukosa huduma za magonjwa ya dharura na ajali kwa wakati, vitaepukwa ikiwa Serikali itasomesha zaidi wataalamu na kuanzisha vitengo vya huduma hiyo kwa kila hospitali nchini.

Wataalamu bingwa waliosomea fani hiyo nchini ni 27 pekee huku wengine tisa wakitarajiwa kuhitimu masomo yao mwaka huu.

Akizungumza katika ufunguzi wa kongamano la Chama cha Watoa Huduma za Dharura Tanzania (EMAT), Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Mpoki Ulisubisya alisema Serikali imejidhatiti kuhakikisha inaongeza wataalamu ili kudhibiti vifo hivyo.

“Takriban asilimia 40 ya wagonjwa hupotea kutokana na uduni wa huduma hii, lazima tuhakikishe asilimia hii hawafariki dunia katika mazingira yetu ya kutolea huduma, hivyo si mikakati tu ya kujenga bali pia kusomesha wataalamu katika fani ya magonjwa ya dharura kwa kadri fedha zinavyopatikana,” alisema Dk Mpoki.

Mkuu wa Kitengo cha Dharura kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Dk Juma Mfinanga alisema changamoto kubwa wanayokumbana nayo wataalamu kwa sasa wagonjwa wa ajali ni wengi.

Alisema kwa Muhimbili kati ya wagonjwa wanaowaona kwa siku, zaidi ya asilimia 25 ni wa ajali na kwamba hiyo ni changamoto waliyonayo japokuwa Serikali inapambana namna ya kupunguza ajali hapa nchini.

Alisema awali walikuwa wakipokea wagonjwa 100-120 lakini kwa sasa inapokea 200-250 kwa siku ambao ni wastani wa wagonjwa 70,000 kila mwaka huku asilimia yao kubwa ni magonjwa ya ajali.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Dk Upendo George alisema EMAT ikishirikiana na MNH, MUHAS na wadau wengine, imetoa mafunzo ya siku mbili kwa washiriki zaidi ya 250 kutoka hospitali mbalimbali kutumia vifaa vichache vilivyopo kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura.