Mbivu, mbichi kesi ya Wema Julai 16

Muktasari:

Awali, Wema alikubali kuwa nyumbani kwake palikutwa na msokoto unaodhaniwa kuwa ni bangi 

Dar es Salaam.  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Julai 16, 2018 itatoa hukumu kesi ya kutumia dawa za kulevya inayomkabili mcheza filamu wa Tanzania, Wema Sepetu na wafanyakazi wake wawili.

Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba anatarajia kutoa hukumu hiyo Julai 16 baada ya mawakili wa upande wa utetezi, Albert Msando na wa upande wa mashtaka Costantine  Kakula kuwasilisha hoja za majumuisho katika kesi hiyo za kushawishi mahakama iwaone washtakiwa hao wana hatia  au la.

Hatua hiyo imefikiwa mahakamani hapo  leo Juni 19 baada ya Wema na wafanyakazi wake, Angelina Msigwa (23) na Matrida Abas (19) wakiongozwa na wakili Msando kujitetea na kufunga ushahidi wao.

Awali, Wema alikubali kuwa nyumbani kwake palikutwa na msokoto unaodhaniwa kuwa ni bangi jikoni, vipisi ambavyo hajui nini katika chumba cha kuhifadhia nguo zake,pochi na viatu na kiberiti katika chumba wanacholala wanamuziki wawili Jodarn na Mila .

Akiongozwa na wakili Msando kujitetea, Wema alieleza kuwa yeye hajui vitu hivyo ni vya nani  kwa sababu yeye ni msanii wa filamu na nyumbani kwake wanaingia watu tofauti tofauti.

Amesema kwa kawaida huwa anafanya sherehe na kualika watu katika nyama choma na chakula cha mchana.