Hatma ya mtangazaji wa Shilawadu kujulikana Septemba 27

Muktasari:

  • Hatma ya watuhumiwa watatu mtangazaji wa kipindi cha Shilawadu, Sudi Kadio (Soudy Brown), Maua Sama na meneja wake Fadhili Kondo wanaoendelea kushikiliwa na polisi kwa siku tisa kujulikana kesho Septemba 26 baada watuhumiwa wengine kufikishwa mahakamani jana na kupata dhamana


Dar es Salaam. Hatma ya mtangazaji wa kipindi cha Shilawadu, Sudi Kadio (Soudy Brown), Maua Sama na meneja wake Fadhili Kondo kujulikana kesho Jumatano, Septemba 26 baada ya kusota kituoni kwa siku tisa.

Akizungumza na Mwananchi wakili Jebra Kambole anayewatetea, “Bado wateja wangu wanashikiliwa ingawa wengine wamefikishwa ila wapo wanaoendelea kushikiliwa kwakuwa tayari maombi yetu yameshawasilishwa mahakamani na kupangiwa kusikilizwa kesho (Jumatano Septemba 26) basi tusubiri uamuzi wa Mahakama.”

Septemba 21 Kambole aliwasilisha maombi Mahakama ya Kisutu dhidi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalum (ZCO) kuwapa dhamana washtakiwa au kuwafikisha mahakamani.

Hata hivyo maombi hayo yalisikilizwa Septemba 24 Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi na kuamuru upande wa mashtaka kuwasilisha majibu na kupanga kusikilizwa Septemba 26 pamoja na washtakiwa hao kuwepo.

Waleta maombi hayo ni Maua Sama, Michael Mlingwa, Fadhili Kondo, Shafii Dauda ,Sudi Kadio, Antony Luvanda na Benedict Kadege

Tayari Michael Mlingwa, Shafiih Dauda, Antony Luvanda, Benedikt Kadege na John Lusingu wameshafikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka yakiwemo kusambaza maudhui mtandaoni bila kibali, ambapo Soudy Kadio, Maua Sama na Fadhili Kondo wakiendelea kushikiliwa kwa tuhuma za kuharibu mali.

Soma Zaidi: