Mbowe ampandisha jukwaani mke wa mgombea kuomba kura

Muktasari:

  • Wananchi wakiwa na mabango wasema watampigia hata kama yupo gerezani.

 Mke wa mgombea udiwani Kata ya Mhandu (Chadema), Godfrey Misana amelazimika kupanda jukwaani kumwombea kura mume wake aliye mahabusu kutokana na kukabiliwa na shtaka la kujeruhi.

Katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika leo Jumapili Novemba 19,2017 katika uwanja wa Shule ya Msingi Mhandu, mwanamama huyo, Rose aliitwa jukwaani na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ili kuomba kura kwa ajili ya mume wake. 

Rose aliwaomba wakazi wa kata ya Mhandu kumpa kura mume wake ili aweze kuwatumikia na kutatua changamoto zote zilizopo katani hapo zikiwamo za barabara, zahanati na maji.

Misana (46), mgombea udiwani wa Chadema katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Novemba 26,2017 na kampeni meneja wake, Charles Chinjibela (37) Ijumaa Novemba 17,2017 walipandishwa kizimbani

wakidaiwa kumjeruhi meneja wa kampeni za CCM katika kata hiyo, Thomas Warioba.

Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza, mbele ya hakimu Ainawe Moshi wanadaiwa kutenda kosa hilo Novemba 14,2017. Mahakama itatoa uamuzi kuhusu dhamana Novemba 21,2017.

Akiomba kura, Rose amemuomba Warioba ambaye ni mlalamikaji katika kesi hiyo kuiomba Mahakama imwachie mume wake kwa kuwa amemkumbuka pamoja na familia yake.

"Nikuombe Warioba uwaambie Mahakama wamwachie mume wangu kwa kuwa mimi na familia yangu tumemkumbuka sana ni siku ya tano sasa hatujamuona, kitanda kimekuwa kikubwa jamani niko chini ya miguu yako mwache mume wangu,” alisema Rose huku akishangiliwa na wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo.

Mbali ya Rose kuomba kura, wananchi walijitokeza na mabango yaliyoandikwa “Hata kama upo gerezani kura tutakupa tulia hivyo hivyo."

Imeandikwa na Kalunde Jamal, Ngollo John na Johari Shani.