Mbowe ashindwa kufika mahakamani, apelekwa nje ya nchi kwa matibabu

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa kuwa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameshindwa kufika mahakamani kwa kuwa amesafirishwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana ilielezwa kuwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameshindwa kufika mahakamani hapo kwa kuwa amepelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

Akitoa maelezo mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, mdhamini wa Mbowe, Grayson Celestine alidai kuwa amepewa taarifa za ugonjwa wa Mbowe na mke wa mwanasiasa huyo.

Awali, wakili wa Serikali mkuu, Faraja Nchimbi aliiomba Mahakama kutoa amri ya kumkamata Mbowe ili ajieleze kwa nini dhamana aliyopewa isifutwe kwa kushindwa kufika mahakamani.

Nchimbi alitoa maelezo hayo baada ya washtakiwa wengine wanane kwenye kesi hiyo ya jinai namba 112, 2018 kupanda kizimbani na Mbowe kukosekana ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo.

Wakili wa Mbowe, Peter Kibatala alianza kwa kuiarifu Mahakama kuwa mdhamini wa mwanasiasa huyo yupo mahakamani hapo.

Akitoa maelezo hayo, Celestine alisema jana aliwasiliana na mke wa Mbowe ambapo alimfahamisha kuwa kiongozi huyo wa kambi rasmi ya upinzani bungeni amesafirishwa kwa ajili ya matibabu ya dharura kutokana na matatizo ya moyo na shinikizo la damu.

“Kwa mujibu wa maelezo ya mkewe, Mbowe anasumbuliwa na moyo na presha (shinikizo la damu) na familia imemsafirisha kwa dharura, lakini mimi sijaonana naye,” alisema Celestine.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mashauri alimuuliza kama ana chochote cha kuithibitishia Mahakama kuwa Mbowe amesafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

Celestine aliieleza Mahakama kuwa mshtakiwa akirejea atawasilisha nyaraka za safari na matibabu, na hadi jana alikuwa akiendelea kufanya naye mawasiliano ili azitume nyaraka hizo kwa njia ya mtandao.

Baada ya kusikiliza maelezo hayo, Wakili Nchimbi alidai mdhamini hajaonyesha uzito wowote kwa kuwa hajaeleza Mbowe amekwenda nje ya nchi lini, katika taasisi gani na nchi gani.

“Labda aliondoka akiwa mahututi lakini waliomsindikiza wangeweza kumdhamini. Sisi upande wa mashtaka hiyo tunaona ni mwendelezo wa dharau ya mshtakiwa namba moja ambaye ni Mbowe kwa Mahakama kwa kuwa alishapewa onyo,” alisisitiza.

Wakili huyo alidai kuwa Mbowe aliamua kwa utashi wake kukiuka amri ya Mahakama.

Hata hivyo, Hakimu Mashauri alisema iwapo mshtakiwa hatapeleka kielelezo chochote, atatoa amri ya kumkamata ili ajieleze kwa nini asifutiwe dhamana kwa kukiuka masharti ya dhamana aliyopewa na Mahakama.