Mbunge ahoji Serikali kukusanya kodi, kushindwa kutoa fedha za maendeleo

Mbunge wa Monduli, Julius Kalanga akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Asema Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina na naibu wake, Abdallah Ulega ni marafiki zake lakini wameshindwa

 


Dodoma. Mbunge wa Monduli (Chadema), Julius Kalanga ameihoji sababu za  Serikali kukusanya kodi kwa wafugaji lakini haipeleki fedha za maendeleo.

Akizungumza leo Mei 17, 2018 katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi mwaka 2018/19, Kalanga amewataja mawaziri wa wizara hiyo, Luhaga Mpina na Abdallah Ulega na kusisitiza, “Ni marafiki zangu na pia ni vijana lakini wameshindwa kabisa.”

Amesema Tanzania kuna makundi manne ya wakulima, wavuvi, wafugaji na wafanyakazi lakini katika kipindi cha miaka mitatu, hakuna mishahara iyopandishwa wala kutolewa fedha za ruzuku kwa wafugaji.

“Fadhila mnazotupa ni zipi? Kwanini mnashindwa kuleta fedha, tumewakosea nini tuwaombe radhi, miaka yote hamjaleta ruzuku, mnakusanya kodi mnashindwa kuturudishia hata kidogo.”

“Hakuna dawa, hakuna ruzuku tunataka kuuza nje (mazao) mnatuzuia, kwa nini? Mnataka kuvuna bila kupanda, mnatuzuia kupeleka nje tupeni masoko, hamtaki, sasa mnataka nini.”