Mchele wa magendo ni jipu kama sukari

Muktasari:

Wakati Serikali ikiendelea kupambana na jipu la sukari kutoka nje, uchunguzi mpya wa Mwananchi umebaini kuwapo wafanyabiashara wanaoingiza mchele usio na ubora kwa magendo kutoka nje na kisha kuuchanganya na ule unaozalishwa nchini ili kuwa na thamani.

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea kupambana na jipu la sukari kutoka nje, uchunguzi mpya wa Mwananchi umebaini kuwapo wafanyabiashara wanaoingiza mchele usio na ubora kwa magendo kutoka nje na kisha kuuchanganya na ule unaozalishwa nchini ili kuwa na thamani.

Uchunguzi huo uliofanywa kwa mwaka sasa, umebaini kuwa mchele huo ukiwamo unaopaswa kupita kwenda nje, huuzwa katika masoko ya ndani baada ya kuchanganywa na unaozalishwa nchini.

Mchezo huu wa baadhi ya wafanyabiashara kutafuta faida chekwa kwa njia chafu, huathiri soko la mchele unaozalishwa nchini.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amekiri kwamba kuna bidhaa zisizolipiwa kodi katika bandari bubu za mwambao wa Pwani.

“Ni kweli suala hilo tunalijua ndiyo maana sasa tunapambana na magendo hayo kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi. Tunawaomba wananchi watoe taarifa wanapoona uhalifu huo, ili tuudhibiti,” alisema Waziri Mwijage.

Kamishna wa Kodi za Ndani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuf Salum alisema mamlaka hiyo imejizatiti kupambana na biashara za magendo kwenye bandari bubu.

“Unajua tumedhibiti sana ukwepaji kodi katika bandari rasmi, ndiyo maana wafanyabiashara wengi wanakimbilia kwenye bandari bubu. Hivi karibuni Mamlaka imechukua hatua kali kwa kuwakamata baadhi ya wafanyabiashara wanaotumia bandari hizo kukwepa kodi,” alisema Salum.

Hata hivyo, msemaji wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Richard Kasuga alisema biashara ya mchele ni huria kama zilivyo nyingine. “Hatujazuia mtu kuingiza mchele au bidhaa yoyote ya chakula nchini. Kitu cha msingi wanatakiwa kulipa asilimia 75 ya kodi.

“Mtu yeyote anaruhusiwa kuingiza mchele kwa kuwa ni biashara huria, kwa hiyo kama mtu anaona inampa faida hakatazwi. Ni kama biashara za maji, juisi, magari na nyinginezo,” alisema Kasuga.

“Si jukumu la Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kutoa vibali vya biashara ya chakula, labda kama kuna baa la njaa. Kwa sasa chakula kipo cha kutosha hakuna haja ya kutoa vibali.”

Ofisa Biashara wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Christopher Nassari alisema jukumu la wizara hiyo ni kutoa leseni za wafanyabiashara bila kujali wanaagiza vyakula aina gani.

Meneja uboreshaji na uhakikisho katika Kitengo cha Forodha TRA, James Mbunda alisema kuna wafanyabiashara walioruhusiwa kuingiza mchele na hulipa kodi. Katika kipindi cha mwaka 2013/ 2014 Tanzania iliingiza tani 22,231.8 na mwaka 2014/2015 mchele ulioingizwa ulifikia tani 32,661.2 wote kwa jumla uliingiza ushuru wa Sh29 bilioni.

Pia, Tanzania ilisafirisha mchele wa tani 68,962.595 mwaka 2013/2014 na tani 24,600.330 mwaka 2014/2015 wote ukiwa na ushuru wa Sh58 bilioni. “Mchele unaoingizwa kwa lengo la kusafirishwa nje ya nchi tunaufuatilia kwa njia ya ‘cargo tracking system’ kuhakikisha unafikishwa unakokwenda,” alisema Mbunda.

Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Gaudencia Simwanza alisema ofisi yake haijawahi kusikia kitu kama hicho, hivyo apewe muda wa kufuatilia.

 

Umoja wa forodha

Ili kutekeleza Itifaki ya Umoja wa Forodha ya Afrika Mashariki, nchi wanachama ziliondoa ushuru wa forodha kwa bidhaa zote zinazokidhi vigezo vya uasili na kupewa cheti cha uasili. Bidhaa hizo, ukiwamo mchele, hazitozwi ushuru wa forodha zinapouzwa ndani ya Jumuiya tangu Januari 2010.

Hata hivyo, Rwanda na Uganda zimerejesha ushuru huo ambao ni asilimia 75 kwa mchele kutoka Tanzania kwa kukosa imani nao.

Meneja Mipango wa Baraza la Nafaka Rwanda, Ikunda Terry alisema Juni mwaka jana kwamba hatua hiyo inalenga kuwabana wafanyabiashara wa mchele wa Tanzania ikithibitika kwamba wamechanganya na ule usio na viwango kutoka Asia.

 

Kauli ya wakulima

Mkulima wa mpunga wa Mbarali – Mbeya, Loveness Stephano alisema japo mchele wa nje haujaingia kwenye masoko ya mkoa huo, lakini unawaathithiri wengi wanaosafirisha zao hilo nje ya mkoa.

“Huku Mbarali mchele kutoka nje ya nchi haufiki, lakini wakulima wetu na wafanyabiashara wanaoupeleka Dar es Salaam ndiyo wanaokumbana na hali hiyo.

Mwenzake, Daina Mwaisabila anaongeza kuwa wameathiriwa na mchele unaotoka nje ya nchi hasa katika masoko ya Dar es Salaam wanakouzia mchele wao.

“Mchele wetu una kiwango cha juu cha ubora ndiyo maana tunauza bei ya juu. Bei zetu zinaanzia Sh1,500 hadi 1,650 kwa kilo. Zamani tulitegemea Soko la Tandale, lakini kwa sasa kuna vituo vingi, unaweza kuuza kuanzia Chalinze, Mlandizi, Kibaha, Kimara, Mwananyamala, Tandika, Mbagala na hata Kigamboni. Lakini kwa kweli mchele wa Pakistan na Thailand unatuathiri kwa kiasi kikubwa,” alisema.