Meya, DED wagongana sakata la wamachinga

Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba

Muktasari:

  • Kibamba amesema hayo wakati akizungumzia uamuzi uliopingwa na Meya wa jiji hilo, James Bwire kuwa baraza la madiwano halikuhusishwa katika kuwatimua wafanyabiashara ndogo maarufu kama wamachinga katika maeneo ya pembezoni mwa mji.

Mwanza. Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba amesema hawajibiki kwa madiwani pekee katika masuala yanayohusu kazi zake, bali anaripoti pia kwa mkuu wa wilaya na wa mkoa.

Kibamba amesema hayo wakati akizungumzia uamuzi uliopingwa na Meya wa jiji hilo, James Bwire kuwa baraza la madiwano halikuhusishwa katika kuwatimua wafanyabiashara ndogo maarufu kama wamachinga katika maeneo ya pembezoni mwa mji.

“Licha ya kusimamia taratibu na sheria, ninawajibika kwa mkuu wa wilaya na wa mkoa, siyo kwa madiwani pekee kama baadhi yao wanavyodhani. Hivyo, ieleweke kuwa mgambo kuwandoa machinga au mamalishe katika kata za Buhongwa na Mahina halihitaji ruhusa kutoka kwa madiwani pekee,” amesema Kibamba.

Hata hivyo, meya wa jiji ameibuka akisema kuwa madiwani hawakupitisha pendekezo la kuwaondoa kwa nguvu wamachinga na mamalishe wanaofanya biashara kwenye barabara na masoko yaliyopo pembezoni mwa jiji.

Bwire ambaye tangu Aprili mwaka jana amekuwa akisafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu baada ya kuvuta hewa iliyodaiwa kuwa na sumu ofisini kwake, alitoa kauli hiyo wiki iliyopita kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Mahina.

“Maana sisi madiwani hatujawahi kupitisha azimio kuwa machinga au mamalishe waondoshwe kando ya barabara kwenye kata ambazo zipo karibu na mji,” alisema Bwire wakati akijibu swali la mkazi wa Ihago, Asteria Petro.

Kwa mujibu wa Bwire, madawani walipendekeza kuhamishwa kwa mamalishe na wamachinga wanaofanya biashara kandokando mwa barabara za katikati ya jiji pekee zikiwamo kata za Nyamagana, Pamba, Mbugani na Mabatini.