Sunday, October 22, 2017

Mganga wa kienyeji adaiwa kunajisi watoto

 

By Gasper Andrew, Mwananchi gandrew@mwananchi.co.tz

Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida, linamshikilia mganga wa kienyeji mkazi wa Mtaa wa Minga, Kata Mitunduruni kwa tuhuma ya kuwanajisi watoto 14 wenye miaka kati ya saba na 12 na kuwasababishia maumivu.

Inadaiwa mtuhumiwa huyo alikuwa akishirikiana kutenda vitendo hivyo na mtoto wa mdogo wake ambaye ni dereva.

Kaimu Kamanda Jeshi la Polisi mkoani hapa, Isaya Mbughi alisema mtuhumiwa anadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Desemba 2016 na Oktoba mwaka huu.

Alisema mganga huyo alikuwa akitumia mbinu ya kuwaonesha picha za video watoto wa kike kisha kuwanajisi.

“Wakati watoto hao wakiendelea kuangalia video sembuleni, mtuhumiwa huyo alikuwa akimchomoa mmoja na kuingia naye chumbani na kumwingilia kimwili na kumpa Sh200 au Sh2,000,” alisema.

Alifafanua kuwa mwathiriki mmoja (jina tunalo) mwenye umri wa miaka saba, wakati akiogeshwa na mama yake Oktoba 16 mwaka huu, saa 11.45 jioni alilalamika kusikia maumivu katika sehemu zake za siri.

Alisema baada ya binti kuyo kulalamika, mama yake alimchunguza na kubaini kuwa na michumbuko katika sehemu za siri.

“Mama huyo baada ya kuona hivyo alimhoji mtoto wake ambaye alimtaja mganga wa kienyeji,” alisema Mbughi.

-->