Mgombea udiwani kizimbani kwa kujeruhi

Muktasari:

Hakimu amesema Mahakama itatoa uamuzi kuhusu dhamana Novemba 21,2017

 

Mwanza. Mgombea udiwani kata ya  Mhandu (Chadema), Godfrey Misana na kampeni meneja wake, Charles Chinjibela, wamepandishwa kizimbani kujibu shtaka la kujeruhi.

Misana (46) na Chinjibela (37) wanadaiwa kumjeruhi meneja wa kampeni za CCM katika kata hiyo, Thomas Warioba.

Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza, mbele ya hakimu Ainawe Moshi wanadaiwa kutenda kosa hilo Novemba 14,2017.

Akisoma mashtaka katika shauri hilo namba 540/2017, mwendesha mashtaka wa Jamhuri, Elizaberth Barabara amedai leo Ijumaa Novemba 17,2017 kuwa washtakiwa walitumia visu na mawe kumjeruhi Warioba.

Kabla ya kuhamia CCM, Warioba alikuwa mwanachama wa Chadema.

Upande wa Jamhuri umeiomba Mahakama kuzuia dhamana ya washtakiwa kwa kile ilichoeleza ni kwa usalama wao.

Ombi hilo la Jamhuri limepingwa na wakili wa utetezi, Gasper Mwanaliela.

Wakili Mwanaliela amesema dhamana ni haki ya wateja wake na kwamba, kuwanyima kutawazuia kushiriki kikamilifu katika kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani unaotarajiwa kufanyika Novemba 26,2017.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu Moshi amesema Mahakama itatoa uamuzi kuhusu dhamana Novemba 21,2017.

Washtakiwa wamepelekwa mahabusu hadi siku huyo.