Upinzani wasogelea ushindi Sierra Leone

Muktasari:

Kati ya asilimia 75 ya vituo vya kupigia kura ambavyo matokeo yake yamehesabiwa Bio wa chama cha SLPP amepata asilimia 43.4 ya kura akifuatiwa na Samura Kamara wa chama tawala cha APC aliyepata asilimia 42.6.


Freetown, Sierra Leone.  Mgombea urais wa chama cha upinzani, Julius Bio anausogelea ushindi baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza kuwa anaongoza kwa tofauti chini kidogo ya kura 15,000, kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa Jumapili.

Kati ya asilimia 75 ya vituo vya kupigia kura ambavyo matokeo yake yamehesabiwa Bio wa chama cha SLPP amepata asilimia 43.4 ya kura akifuatiwa na Samura Kamara wa chama tawala cha APC aliyepata asilimia 42.6.

Mgombea wa muungano wa NGC unaoongozwa na mwanadiplomasia wa zamani katika Umoja wa Mataifa (UN) Kandeh Yumkella, ambaye anatarajia kuwaharibia vinara wawili hao, alipata asilimia 6.69.

Matokeo kamili yanatarajiwa kutangazwa siku chache zijazo, lakini kwa mwelekeo huu kuna kila dalili za kufanyika raundi ya pili kutokana na ukweli kwamba hakuna kati ya vinara hao anayeweza kufikia asilimia 55 katika duru ya kwanza.

Rais Ernest Bai Koroma ambaye hakuweza kugombea tena tena baada ya kukamilisha vipindi vyake vya uongozi alimtia mafuta Kamara kuwa mrithi wake kupitia chama tawala cha All Peoples Party (APC).

Vyama vya APC na Sierra Leone Peoples Party (SLPP) cha Bio ndivyo vimekuwa vikipokezana uongozi wan chi tangu Sierra Leone ilipojinyakulia uhuru wake kutoka Uingereza mwaka 1961.

Waangalizi wa uchaguzi huo kutoka Umoja wa Ulaya Ijumaa walitoa ripoti yao ya awali iliyosema uchaguzi huo kuwa wa “uwazi, kuaminika na ulioandaliwa vizuri” kwa ujumla.