Miaka mitatu ya Magufuli na malengo magumu aliyojiwekea

Muktasari:

Pamoja na kwamba hii ni nguzo muhimu ambayo Rais Magufuli na wasaidizi wake wameisimamia katika miaka hii mitatu, Profesa Jala anasema ukishaweka malengo na vipaumbele vyako haitoshi.

Karibuni tena katika mfululizo wa makala hizi kuelekea miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dk John Pombe Magufuli.

Wiki iliyopita nilifanya bashrafu (utangulizi) iliyogusia baadhi ya nguzo muhimu za mafanikio katika awamu hii inayofikisha miaka mitatu Novemba 5 mwaka huu.

Niliahidi kuwa tutaanza kuchambua maeneo muhimu makubwa ya kiutekelezaji, ili tulipotoka katika miaka hii mitatu, tulipo na tunapotaka kwenda.

Hata hivyo, leo nitamalizia kwa kujadili msingi mwingine, ambao binafsi naamini ni nguzo nyingine muhimu tunapojadili mageuzi katika miaka hii mitatu.

Kwa sababu ya uumini wangu wa mageuzi, nimekuwa nikisoma vitabu vingi vinavyoonyesha namna viongozi na hata wanaharakati wakubwa duniani walivyopambana kuleta mageuzi katika jamii zao.

Ukiacha Mwalimu Julius Nyerere, mwalimu wa wengi, nimejifunza pia kutoka kwa viongozi wengi duniani.

Kwa mfano, nimejifunza kutoka kitabu cha James Brown kiitwacho: “The Life and Times of Mahatma Gandhi” nikajifunza namna utulivu, uvumilivu na nguvu ya kiroho inavyoweza kuwa chagizo la mageuzi makubwa katika jamii.

Nikaenda mbali zaidi kumsoma mwandishi Said K. Aburish katika “Arafat: From Defender to Dictator” akizungumzia zaidi harakati na kukwama kwa aliyekuwa kiongozi wa Wapalestina Yasser Arafat aliyewaongoza walau kuunda taifa lao la ndani.

Nikajifunza ‘stratejia’ katika mageuzi hasa wakati wa changamoto nyingi.

Nikaenda mbali zaidi kwa kumsoma Mzee Nelson Mandela katika “The Long Walk to Freedom”

Kutoka Mashariki ya Mbali, sikuacha kuchota ujuzi kutoka kiongozi wa Singapore Lee Kuan Yew katika andiko lake “From Third World to First-The Singapore Story 1965 hadi 2000.”

Kote huko na kwingine ambako si rahisi kuorodhesha uzoefu wote nilioupata, kuna kubwa moja la kujifunza ambalo ni maana ya mageuzi katikati ya upinzani mkubwa; upinzani unaojaribu kuzuia mageuzi ya kweli.

Hata hivyo, nikiri kuwa pamoja na kuwasoma wanamageuzi hao wote na nadharia nyingi za uongozi nilizojifunza, nimeguswa sana kutoka uzoefu wa mwanamageuzi wa Kimalaysia, Profesa Idris Jala.

Katika dhana yake ya “Six Secrets of Transformation” Profesa Jala anashadidia namna Malaysia (kama ilivyokuwa kwa Singapore), ilivyotumia siri hizo sita kufika ilipo leo.

Ikumbuke kuwa taifa lililotoka katika lindi la umaskini miaka ya 1960 hadi kuwa Taifa la kisasa la viwanda, teknolojia na kila aina ya utoaji wa hali ya juu wa huduma za jamii. Nitajadili siri mbili kati ya hizo.

Miaka mitatu ya malengo

Profesa Jala anaamini kuwa viongozi wenye damu ya kimageuzi kwanza huweka bayana malengo na vipaumbele vyao.

Alipoingia madarakani, Rais Magufuli alitoka kuinadi Ilani ya chama Chama cha Mapinduzi (CCM), iliyokuwa na orodha ndefu ya mambo ya kufanya.

Katikati ya orodha hiyo, aliweka bayana vipaumbele vyake kama vile kukusanya kodi, kuondoa mianya ya rushwa, kupambana na uzembe kazini na kupunguza matumizi ya anasa serikalini, ajenda yake kuu ya ‘Tanzania ya Viwanda’ na vinginevyo.

Pamoja na kwamba hii ni nguzo muhimu ambayo Rais Magufuli na wasaidizi wake wameisimamia katika miaka hii mitatu, Profesa Jala anasema ukishaweka malengo na vipaumbele vyako haitoshi, anasema viongozi wanaofanikiwa si tu ni wale wanaoweka malengo, bali pia ni wanaoweka malengo makubwa na magumu, ambayo ameyaita Kiingereza kwa jina la ‘Olympic Targets’

Miaka mitatu ya malengo magumu

Akishadidia siri hii, Profesa Jala anasema katika lugha ya Kiingereza: “Create a game so large that it can consume you,” kwamba viongozi wanamageuzi huweka malengo magumu kiasi kwamba yanaweza kuwagharimu (kwa kulaumiwa kuwa ni ndoto tu au hayatekelezeki).

Katika miaka hii mitatu Rais Magufuli amedhihirisha kuwa yeye ni mwanamageuzi wa karne ya 21.

Amejiwekea malengo magumu kiasi kwamba kama anavyosema Profesa Jala wapo waliosema na wanaojaribu kudhani hatayatekelezeka.

Miaka ya 2010-2015 kulikuwa na kilio cha nchi yetu kutokuwa na ndege hata moja.

Nakumbuka mbunge mmoja aliwahi kuhoji; ‘‘Ni nchi gani hii haina hata kandege kamoja? Magufuli alipoingia akaweka lengo gumu, wengi wakasema hataweza kuifufua ATCL

Ndani ya miaka mitatu, Rais Magufuli ametuvika nguo kimataifa, ndege kadhaa ziko angani.

Januari 27, 2013 nikiwa mmoja wa maofisa waandamizi katika Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM), nilikuwepo jijini Addis Ababa, Ethiopia. Tanzania iliwasilisha ripoti yake iliyosheheni maoni ya wananchi na ya wataalamu kutoka mataifa mengine ya Afrika kuhusu hali ya utawala bora. Swali moja kubwa lilihusu Tanzania inafaidikaje na madini?

Miaka mitatu leo, maono ya APRM yamefanyiwa kazi. Manufaa ya mageuzi katika sekta ya madini ni mengi, makubwa na yanatia moyo. Usibanduke katika safu hii kuna kitu cha maana kwako Mtanzania nitakujuza. Hakijaelezwa bado. Lengo gumu, limetekelezwa.

Kuna mwanasiasa mmoja wa Kigoma alipata kuwa maarufu sana kwa kuipigia debe na kuipigania reli ya kwenda Kigoma.

Alifika hatua hata ya kuwahi, (naamini kwa utani), kutamani Kigoma ijitenge maana imesahaulika kuboreshewa reli. Rais Magufuli akaja, akaahidi kuboresha reli hasa ile ya kisasa. Leo kazi imeanza na iko asilimia 20.

Ahadi ya reli ya kisasa ilionekana kuwa ni mradi mgumu kutekeleza na labda upatikane msaada kutoka nje ya nchi. Lakini Rais Magufuli alipambana na hofu zote hizo za kushindwa.

Yako mengi labda nimalizie kwa hili: kama kuna eneo Serikali inapokea kelele kutoka kwa wawekezaji na wananchi ni hoja na haja ya nishati zaidi ya umeme.

Juhudi mbalimbali zimechukuliwa tangu enzi za Baba wa Taifa kwa kuwekeza katika umeme wa maji ambao uliendelezwa katika awamu ya pili na ya tatu.

Alipoingia Rais Magufuli aliendelea kupambana na kero hii kwa nguvu zote, ikiwamo kuutekeleza mradi ambao hata Mwalimu Nyerere alitamani lakini akashindwa kwa sababu ya gharama.

Huu ni mradi wa megawati 2,100 wa Stiglers. Ilipotajwa Stiglers, kama kawaida, hofu zikaibuka.

Wakati hofu zikiendelea akaanza na mradi wa nyongeza wa Kinyerezi I (K-I extension) utakaozalisha megawati 185 ambao umefikia nusu, huku muda wowote kutoka sasa pia ikitarajiwa mradi wa umeme wa gesi wa K-II utakamilika na kuingiza megawati nyingine 280 kufikia mwishomi mwa waka huu.

Ni ahadi kubwa kama hizi za kimageuzi ambazo zinawafanya Watanzania wengi waone fahari ya kuwa sehemu ya safari hii; safari ambayo unaruhusiwa kujiunga nayo wakati wowote-sasa au hata kesho.

Sisi tulioianza safari hii tunawakaribisha, na nakuthibitishia katika safari hii ya mageuzi haya, hakutakuwa na kurudi nyuma wala kusalimu amri.

Hadi wiki ijayo, alamsiki.

Dk Hassan Abbasi ni msemaji mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Anapatikana kupitia baruapepe: [email protected].