‘MO’, TBL nani ni nani Simba

Mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji ‘MO’ .

Muktasari:

  • Tetesi hizo zinakuja baada ya kuwapo kwa mpango wa mwanachama na mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji ‘MO’ kutaka kuinunua klabu ya hiyo.
  • Hivyo,mpango huo umeiweka njiapanda TBL katika udhamini wake kwenye klabu hiyo kongwe nchini.

Dar es Salaam. Kuna taarifa kuwa  Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) huenda ikajiweka kando katika kuidhamini timu ya Soko ya Simba baada ya kumaliza mkataba wao, baadaye mwaka huu.

Tetesi hizo zinakuja baada ya kuwapo kwa mpango wa mwanachama na mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji ‘MO’ kutaka kuinunua klabu ya hiyo.

Hivyo,mpango huo umeiweka njiapanda TBL katika udhamini wake kwenye klabu hiyo kongwe nchini.

Kitendo cha Dewji kutaka kununua hisa nyingi Simba, kumetajwa kuwa chanzo cha TBL kutaka kujiweka kando na udhamini huo huku Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, Pamela Kikuli akisisitiza kuwa kampuni yao kutokuwa katika nafasi ya kulisemea suala hilo kwa sasa.

“Ninasema TBL kwa sasa hatuko kwenye nafasi ya kuzungumzia suala hilo kama tutaendelea kuidhamini Simba au la, wakati ukifika tutazungumza,” amesema meneja.

TBL imekuwa ikiidhamini Simba sanjari na Yanga kwa muda mrefu, ingawa kuna taarifa za kampuni hiyo kutaka kujiweka kando na udhamini huo baada ya kumaliza mkataba wao baadaye mwaka huu.