Beki Mzimbabwe wa Simba asubiri kurudi ‘kwao’ Mbeya

Method Mwanjali

Muktasari:

Mwanjali ataongozana na wenzake hadi Mbeya, Oktoba 8 ili kucheza na Prisons, akieleza kuwa asili yake kwenye mkoa huo inamwongeza hamu ya kusafiri kwenda huko.

Wakati beki wa kati wa Simba, Mzimbabwe Method Mwanjali akisema anasubiri kwa hamu safari ya Mbeya kucheza mechi za Ligi Kuu, mahali ambako ni asili yake, benchi la ufundi la klabu hiyo linakabiliwa na kibarua cha kusaka mabao.

Mwanjali ataongozana na wenzake hadi Mbeya, Oktoba 8 ili kucheza na Prisons, akieleza kuwa asili yake kwenye mkoa huo inamwongeza hamu ya kusafiri kwenda huko.

Alieleza kuwa yeye ni Mnyakyusa wa Mbeya, mzaliwa wa Vwawa, Mbozi katika mkoa mpya wa Songwe, ila wazazi wake walihamia Zimbabwe.

Alisema aliishi Vwawa akiwa mdogo pamoja na babu yake lakini familia yao ilihamia Zimbabwe alikokulia na kucheza kwa mafanikio kwenye timu ya taifa pamoja na Ligi ya Afrika Kusini.

Aliliambia gazeti hili juzi kuwa yeye ni mzawa, kwao ni Vwawa, Mbozi, mahali ilikotoka familia yao, ambayo baadaye ilihamia Zimbabwe.

“Nilishawahi kuishi Mbeya miaka ya nyuma, niliondoka nikiwa na miaka mitatu na mwaka 1995 nilikuwa huko.

Kwa sasa, babu anaishi Zimbabwe,” alisema Mwanjali, akiunga na kauli ya rais wa klabu hiyo, Evance Aveva aliyewahi kuliambia gazeti hili kwamba amekuwa akiwasiliana na beki huyo kwa Kinyakyusa.

Mbali ya kucheza kama beki ya kati kwenye kikosi cha Simba, anao pia uwezo wa kucheza kama kiungo. Amekubalika Simba kutokana na uelewano wake mzuri na mabeki wenzake wa kati, Novatus Lufunga, Juuko Murshid na Emmanuel Simwanza.

Wakati Mwanjali akiwaza kwenda Mbeya, mechi mbili za mwanzo za Ligi Kuu ilizocheza Simba zimetosha kuonyesha udhaifu kwenye safu ya ushambuliaji.

Udhaifu huo unalifanya benchi la ufundi lilazimike kurudi darasani kusaka mbinu za kuipa makali safu hiyo ya ushambuliaji inayokumbwa na tatizo la kutofunga mabao kutokana na nafasi inazozitengeneza.

Simba ambayo Jumamosi ilitoka sare ya 0-0 dhidi ya JKT Ruvu ya mkoani Pwani imeonekana kutegemea zaidi krosi na mipira ya adhabu ndogo ili kufunga mabao.

Kabla ya sare ya juzi, timu hiyo iliibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara, bao la kwanza likifungwa kwa faulo na mengine mawili mawili yakitokana na kona.

Hiyo inaashiria kuwa endapo timu pinzani zitaibana ili isipate kona au mipira ya adhabu, timu hiyo itakuwa na wakati mgumu kupata matokeo mazuri.

Kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja alikiri kuwapo kwa tatizo hilo akiahidi kulirekebisha.

“Katika mpira kuna nyakati unaweza kucheza vizuri ukapata matokeo na wakati mwingine ukashindwa. Nakiri ni tatizo, lakini tutalifanyia kazi ilikuhakikisha halijirudii tena mechi zijazo,” alisema Mayanja.

Kipa wa JKT Ruvu, Said Kipao aliliambia gazeti hili kuwa kufahamu mapema udhaifu wa Simba ndiko kuliwasaidia kutoka sare juzi.

“Simba ni timu nzuri, lakini tulishawasoma kupitia mchezo wao na Ndanda tukagundua kuwa tukiwadhibiti kwenye kona, hawawezi kufurukuta na ndicho tulichokifanya,” alieleza kipa huyo aliyeng’ara kwenye mchezo huo. Meneja wa Simba, Musa Hassan ‘Mgosi’ alisema kuwa anaamini watarekebisha udhaifu wao, ingawa ligi ni ngumu.