Dar kumpa ubingwa Lwandamina

Kocha wa Yanga, George Lwandamina

Muktasari:

Kwa kuangalia jiografia ya Tanzania na miundombinu yake, ikiwamo barabara, reli na ndege ambayo inatumika kwa kiasi kidogo, Yanga ina kazi rahisi, ikilinganishwa na mtani wake, Simba kwenye mzunguko huo, kwani itahitaji kusafiri umbali mfupi zaidi.

Dar es Salaam. Mcheza kwao hutuzwa! Ndicho kinachoonekana kwenye ratiba ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara kuisafishia njia Yanga ya kutetea ubingwa wake kwa kuutwaa mara ya tatu, endapo itazitendea haki mechi zake 12 itakazocheza kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa kuangalia jiografia ya Tanzania na miundombinu yake, ikiwamo barabara, reli na ndege ambayo inatumika kwa kiasi kidogo, Yanga ina kazi rahisi, ikilinganishwa na mtani wake, Simba kwenye mzunguko huo, kwani itahitaji kusafiri umbali mfupi zaidi.

Timu hiyo ya Mitaa ya Twiga na Jangwani, ina misuli kifedha kupitia mdhamini na mwenyekiti wake, Yussuf Manji kiasi cha kumudu pia usafiri wa ndege, itasafiri kwa basi umbali wa kilomita 979 kwenda Songea na kurudi, kisha kilomita 196 za barabara kwenda Morogoro na kurudi, itaruka kwa ndege hadi Mwanza, kilomita 1,148 na kurudi Dar es Salaam, ambako itatuliza akili zake ikiwasubiri wageni wake.

Katika mzunguko uliopita iliomaliza ikiwa na pointi 33, Yanga inayochuana na Simba yenye pointi 35 na Azam, pointi 25 ili kusaka taji hilo kwa msimu wa tatu, itacheza mechi tatu pekee nje ya Dar es Salaam, zitakazokuwa dhidi ya Majimaji, Mtibwa na Mbao FC, tofauti na Simba katika mzunguko wa pili.

Simba inazo mechi saba ugenini, sawa na pointi 21 ambazo zitakuwa ngumu kupatikana Mtwara, dhidi ya Ndanda, kisha Mwanza kwa Toto Africans na Mbao FC , Kagera ambako itaumana na wenyeji Kagera Sugar, itasafiri pia kwenda Songea kucheza dhidi ya Majimaji na Morogoro dhidi ya Mtibwa Sugar.

 

Raundi ya pili kwa mtazamo wa wachambuzi

Mwanasoka wa zamani na mchambuzi wa masuala ya soka, Ally Mayay alisema mara nyingi mechi za nyumbani katika mzunguko wa pili wa ligi ndizo zinazotengeneza mazingira ya ubingwa wa Ligi Kuu.

Mayay aliyeichezea Yanga na Taifa Stars alisema mzunguko wa pili ni mgumu na timu zinapambana ili kusaka ubingwa na nyingine kujinasua katika hatari ya kushuka daraja.

“Katika mzunguko wa pili, rekodi ziko hivi, mechi za nyumbani mara nyingi ndizo zinaamua timu ipi iwe bingwa na ipi ishuke daraja kama timu huska zitazitendea haki mechi zake za nyumbani,” alisema Mayay.

Katika mzunguko wa pili, Yanga itacheza na Prisons, Kagera Sugar, Toto Africans, Mwadui, Ndanda, Mbeya City, Stand United, JKT Ruvu, Ruvu Shooting, African Lyon, Azam na Simba kwenye uwanja wa Taifa ambao imeupata kutoka Serikalini.

Baadhi ya mechi Yanga itakuwa ugenini kwa mujibu wa ratiba, lakini kiuhalisia inacheza kwenye uwanja wake wa nyumbani, Taifa.

“Kama Yanga itatumia mechi za nyumbani inayo nafasi ya kutwaa ubingwa mapema, vivyo hivyo kwa Simba, pia hata Azam kwani kati ya timu 16 zinazoshiriki ligi, hizi tatu ndizo zinamalengo ya ubingwa,” alisema Mayay.

Katika mzunguko wa kwanza, Simba ilicheza mechi 10 jijini Dar es Salaam, ilishinda tisa, sare moja na ilicheza mechi tano nje ya Dar es Salaam, ilishinda tatu, sare moja na kufungwa moja. italazimika kwa mfano kusafiri hadi Bukoba, umbali mrefu zaidi , ambao ni kilomita 1,588.

Yanga, tayari imeanza maandalizi ya raundi ya pili ikiwa chini ya kocha mpya George Lwandamina, ambaye msimu wake wa kwanza hatafanya utalii wa ndani kwa kucheza zaidi Dar es Salaam.

Lwandamina ameanza usajili wake kwa kumnasa kiungo Mzambia Justin Zulu atakayeanza kuiongoza naye raundi ya pili akikuta kumbukumbu ya mechi nane ilizocheza timu yake jijini Dar es Salaam, ilikoshinda tano na sare tatu na kucheza mechi saba ugenini, ikashinda nne, kufungwa mbili na sare moja.

 

Pluijm na hesabu za ubingwa

Kwa mtazamo na hesabu hizo, mkurugenzi wa ufundi wa Yanga, Hans Pluijm ameitabiria timu yake (Yanga) ubingwa kwa mara nyingine.

Pluijm ambaye mzunguko wa kwanza alikuwa kocha mkuu kabla ya kumkabidhi kijiti Lwandamina hivi karibuni aliliambia gazeti hili katika mahojiano maalumu kwamba Yanga inajua inachokifanya. “Hakuna timu isiyojiandaa, maana kama hujiandai unajiandaa kushindwa. Sisi tuna timu nzuri na iliyokamilika kila idara, tunaamini maandalizi yetu ni bora na ndio sababu tunaamini tutatwaa ubingwa na kufanya vizuri mashindano ya kimataifa,” alisema na kuongeza.

“Tuna kocha mpya ambaye ameleta changamoto katika timu, hii itaongeza hamasa kwa wachezaji,” aliongeza Pluijm ambaye kwenye mzunguko wa kwanza aliiongoza Yanga kushinda mechi 10, kutoka sare tatu na kufungwa mbili.

 

Mkude ataka umoja Simba

Nahodha wa Simba, Jonas Mkude amekiri timu yao kuingia katika hatua ngumu kwenye mzunguko wa pili hasa kutokana na kucheza mechi nyingi za ugenini lakini akasisitiza, umoja, mshikamano na juhudi vitaisaidia timu yao kutwaa taji hilo msimu huu.

“Tunajua namna Simba inavyohitaji ubingwa, ndoto yangu ni kuona tunafanikiwa katika hilo nikiwa nahodha lakini bila juhudi, mshikamano na umoja mambo yanaweza kuwa magumu kwani tunakoelekea ndiko kugumu zaidi,” alisema Mkude.

“Kwa hali ilivyo, tunahitaji kuongeza juhudi, ushirikiano na umoja ili kutimiza ndoto yetu, tuungane na kuendeleza kauli mbiu yetu ya Simba bingwa msimu huu, tukilegea tutakwama kwani mzunguko unaokuja ndiyo mgumu zaidi, tunahitaji utulivu na umoja kutimiza malengo,” alisema.

Aidha, kiungo huyo wa Simba ambaye amekuwa akitajwa kugomea mkataba mpya na klabu hiyo aliweka wazi hatma yake ndani ya timu hiyo na kusema kwamba hajaamua kuondoka Simba au kubaki licha ya kusisisitiza kuwa bado ni mwajiriwa na Simba kwa mujibu wa mkataba wake ambao hata hivyo umebakiza miezi michache kumalizika.

“Siwezi kusema nitaondoka Simba kienyeji au nitaendelea kubaki, bado mkataba wangu haujakwisha, nikimaliza mkataba kila kitu kitajulikana,” alisema mchezaji huyo ambaye hivi karibuni kulikuwa na taarifa za yeye kuachana na klabu hiyo.