Deni lavuruga mashindano ya Kombe la Kikapu la Nyerere

Muktasari:

  • Mabingwa hao wa Ligi ya Taifa ya Mpira wa Kikapu (NBL) walizuiwa kucheza nusu fainali dhidi ya Oilers.

Dar es Salaam. Mashindano ya Kombe la Mwalimu Nyerere ya mpira wa kikapu yameingia dosari kutokana na timu ya Savio kuzuiwa kucheza kutokana na Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) kusema inadaiwa Sh150,000 za ada ya ushiriki.

Mabingwa hao wa Ligi ya Taifa ya Mpira wa Kikapu (NBL) walizuiwa kucheza nusu fainali dhidi ya Oilers.

Hata hivyo, madai hayo yalipingwa na katibu mkuu wa Savio, Abdulkadir Issa Mtambo akisema klabu yake ilishiriki tangu mwanzo kwa makubaliano ya kukatwa fedha hizo kutokana na deni wanalowadai TBF.

Mtambo alisema klabu yake inaidai TBF dola 600 (Sh1,306,200) walizowakopesha kwa ajili ya kulipa ada ya chama katika shirikisho la mchezo huo Afrika (Fiba) mwaka jana nchini Rwanda.

Alisema baada ya uongozi wa Savio kujua kuwa TBF itawawia vigumu kulipa deni hilo, waliwaita na kukubaliana watakuwa wanakata fedha katika michezo itakayokuwa inaandaliwa na TBF.

TBF walianza kukata fedha katika mashindano ya Ligi ya Taifa ya mchezo huo (NBL) kwa timu za Savio, DB Lioness na Young Stars. Katika mashindano hayo, TBF ilikata Sh525,000 kwa timu hizo tatu.

Akizungumzia mashindano ya Kanda ya Tano ya Afrika, alisema TBF pia iliwatia hasara baada ya kupigwa faini zaidi ya Dola 40 kwa kuchelewesha usajili wa wachezaji katika mashindano hayo.

Alisema uongozi wa TBF ulipaswa kutafuta fomu za usajili kwa timu za Tanzania zinazoshiriki mashindano ya kanda.

Alisema klabu yake ilishughulikia suala hilo na kupata fomu za usajili kwa Savio na DB Lioness.

Wakati huo huo; Kocha mkuu wa timu ya Patriots kutoka Rwanda, Enery Mwinuka amesema kuwa klabu yake haitashiriki na mashindano yeyote nchini chini ya uongozi uliopo.