Ghana yaibuka kidedea

Muktasari:

Kahraba aliingia kipindi cha pili mjini Port-Gentil na kukifungia kikosi cha Misri dakika ya 88, kabla ya mchezo kwenda dakika 30 za nyongeza.

Gabonese, Gabon. Bao la dakika za mwisho la Mahmoud Kahraba limeipa ushindi Misri kuwafunga vijana wa kocha Herve Renard, Morocco katika mchezo wa robo fainali ya Mataifa ya Afrika huku Ghana nayo ikitinga nusu fainali.

Kahraba aliingia kipindi cha pili mjini Port-Gentil na kukifungia kikosi cha Misri dakika ya 88, kabla ya mchezo kwenda dakika 30 za nyongeza.

Ndugu wawili wa familia ya Ayew, Jordan na Andre, wote walifunga kuipa Ghana ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya DR Congo mjini Oyem na kuwapa nafasi ya kucheza nusu fainali.

Renard raia wa Ufaransa alitarajia kuvunja rekodi ya kuwa kocha wa kwanza kutwaa mataji matatu akiwa na timu tatu tofauti baada ya kufanya hivyo akiwa na Zambia 2012 na Ivory Coast 2015.

Lakini badala yake, ilikuwa Misri iliyofanikiwa kupata nafasi ya kucheza nusu fainali, ambayo ipo katika kampeni ya kutwaa taji hilo kwa mara ya nane.

“Ilikuwa ni mechi ngumu kwa timu zote kwa dakika 94. Sote tulikuwa na nafasi lakini tulikosa nafasi na kutumia moja,” alisema Hector Cuper, alisema Kocha wa Misri raia wa Argentina, ambaye kikosi chake hakijafungwa bao katika mechi nne sasa nchini Gabon.

Morocco walikuwa na nafasi kupitia kwa Romain Saiss na M’bark Boussoufa, ambao wote waligongesha nguzo, wakati Aziz Bouhaddouz akishindwa kuunganisha wavuni pasi ndefu ya Faycal Fajr kipindi cha pili.

Misri walikuwa na hatari zaidi kipindi cha pili na nyota wao, Mohamed Salah alinyimwa bao mara mbili na kipa Munir Mohamedi katika lango la Morocco.

Dakika 30 za nyongeza ziliota mbawa baada ya Morocco kushindwa kutumia kona yao langopni mwa Misri dakika mbili kabla ya mchezo kumalizika na Kahraba, ambaye anacheza Saudi Arabia kuamua matokeo.

“Nimefurahishwa na wachezaji wote. Mmoja baada ya mwingine, kiukweli wamefanya kazi kubwa,” alisema Renard licha ya kufungwa.

“Hatutakiwi kujuta. Tunatakiwa kujivunia kwa kile tulichofanya kwa sababu tulipotoka ni mbali.”