Hesabu za Yanga zaweza ipeleka nusu fainali Shirikisho

Kocha wa Yanga, Hans Van Pluijm

Muktasari:

Katika uhalisia, Yanga ambayo inashika mkia katika Kundi A kwa kuwa na pointi moja, ina nafasi finyu kutinga hatua ijayo ya nusu fainali ya mashindano hayo.

Dar es Salaam. Hesabu bado zinapigika kwa Yanga kwenye mashindano ya kimataifa licha ya kupoteza mechi tatu kati ya nne walizocheza hadi sasa.

Yanga inayoshiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, imepoteza mechi dhidi ya MO Bejaia ugenini (1-0), ikafungwa nyumbani na TP Mazembe (1-0), ikalazimishwa sare ya bao 1-1 na Medeama kabla ya timu hiyo ya Ghana kuifunga Yanga mabao 3-1.

Katika uhalisia, Yanga ambayo inashika mkia katika Kundi A kwa kuwa na pointi moja, ina nafasi finyu kutinga hatua ijayo ya nusu fainali ya mashindano hayo.

Ikiwa imebakiza michezo miwili dhidi ya MO Bejaia nyumbani na TP Mazembe ugenini, Yanga bado haijakata tamaa licha ya kuachwa na pointi moja hadi sasa.

Baada ya TP Mazembe kuifunga MO Bejaia bao 1-0 wiki iliyopita, hali imekuwa ngumu kwa miamba hiyo ya Algeria iliyoshika nafasi ya pili tangu kuanza kwa hatua ya makundi.

Kipigo hicho kimefanya kuwa sawa na Medeama kwa pointi tano, hatari ambayo inaweza kuwa mbaya katika kusaka nafasi ya ushindi kwa timu zote hizo mbili zina nafasi.

Lakini hesabu zinazopigwa na Yanga ni kuiombea TP Mazembe kuibuka na ushindi katika mchezo wao ujao nchini Ghana dhidi ya Medeama ili kuibakiza timu hiyo kwa pointi tano.

Wakati wakiliomba hilo, Yanga inatakiwa kushinda michezo yao miwili iliyobaki ili kufikisha pointi saba, wakati mchezo wa mwisho kati ya Medeama na MO Bejaia umalizike kwa sare yoyote.

Kama hilo litafanikiwa, MO Bejaia na Medeama watamaliza wakiwa na pointi sita na Yanga kupata nafasi ya kucheza nusu fainali, lakini linaonekana kuwa gumu.