Tuesday, January 10, 2017

Iwe jua, iwe mvua lazima mmoja afe

 

By Gift Macha, Mwananchi

Zanzibar. Tambo, kejeli, masihara na kucharurana, ndiko kulikotawala kila mahali kuelekea mchezo wa leo usiku wa Simba na Yanga ikiwa ni nusu fainali ya pili ya Kombe la Mapinduzi kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Baada ya Yanga kuchapwa mabao 4-0 na Azam, Yanga hawakulala kwa tambo za Simba, lakini wakajitutumua wakisema tunawataka Simba, lakini wakasema Jang’ombe Boys wanaweza kushinda Simba akacheza na Azam. Sasa ni Simba na Yanga.

Kabla ya mchezo na Jang’ombe Boys, kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja alisema: “Sisi hatupangi matokeo ya kufungwa, atakayekuja mbele tunapiga, hatuogopi mtu.” Sasa Zanzibar itasimama dakika 90 na hapo ndipo tambo na kelele za kila aina zitakapokoma.

Watani hao wa jadi wanakutana ikiwa ni siku 102 baada ya mashabiki wa Simba kung’oa viti kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam katika mchezo wa mwisho wa watani hao uliochezwa Oktoba Mosi mwaka jana.

Mchezo huo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 uliingia dosari baada ya mwamuzi Martin Saanya kukubali bao tata la Amissi Tambwe na kisha kumpatia kadi nyekundu ya utata nahodha wa Simba, Jonas Mkude.

-->