Kambi ya Serengeti Boys yamkuna Kim

Mkuu wa Kitengo cha Ufundi cha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Kim Poulsen

Muktasari:

  • Serengeti Boys ilifuzu kucheza fainali hizo za Gabon baada ya kushinda rufani yake dhidi ya Congo-Brazzaville iliyobainika kumchezesha Langa Lesse Bercy aliyezidi umri wake ulizidi miaka 17.

Dar es Salaam. Mkuu wa Kitengo cha Ufundi cha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Kim Poulsen amepongeza hatua ya kuichagua Morocco kuwa nchi itakayoweka kambi Serengeti Boys ikijiandaa na fainali za Afrika kwa vijana zitakazoanza Mei 21 hadi Juni 4.
Serengeti Boys ilifuzu kucheza fainali hizo za Gabon baada ya kushinda rufani yake dhidi ya Congo-Brazzaville iliyobainika kumchezesha Langa Lesse Bercy aliyezidi umri wake ulizidi miaka 17.
Akizungumza na gazeti hili jana Poulsen alisema timu hiyo itarejea kambini katikati ya mwezi huu kabla ya kwenda Morocco kwa kambi ya mwezi mmoja.
“Hiyo ni kambi muhimu kwetu na tunashukuru taratibu zote zinakwenda vizuri. Vijana wanarejea hivi karibuni, lakini tuna jukumu kubwa la kuwaandaa vizuri hasa kwa kucheza mechi nyingi za kujipima nguvu,” alisema Poulsen.
Kabla ya kwenda Morocco kikosi hicho kinatarajia kucheza mechi za kirafiki dhidi ya Kenya, Rwanda na Guinea.
Timu nne zinazofuzu kwa nusu fainali ya Afcon kwa vijana zinakata tiketi ya moja kwa moja kucheza Kombe la Dunia litalofanyika India.