Kocha Liewig aeleza yaliyomshinda Stand

Patrick Liewig

Muktasari:

  • Kocha Liewig, raia wa Ufaransa alisema kuwapo na mkanganyiko katika usajili na usainishwaji wa mikataba, malipo ya bonasi za wachezaji na utata wa mchezo kati yao na Mbeya City, vilichangia abwage manyanga.

Dar es Salaam. Aliyekuwa kocha wa Stand United, Patrick Liewig amebainisha mambo matatu yaliyomshawishi kuachana na miamba hiyo ya Shinyanga.

Kocha Liewig, raia wa Ufaransa alisema kuwapo na mkanganyiko katika usajili na usainishwaji wa mikataba, malipo ya bonasi za wachezaji na utata wa mchezo kati yao na Mbeya City, vilichangia abwage manyanga.

Katika waraka huo, Liewig alilalamikia kutokuwa na ufanyaji kazi wa kuzingatia uongozi kwa wachezaji kushindwa hata kuwa na nakala za mikataba yao.

Alidai kuwa mikataba hiyo haikusainiwa na wahusika katika ngazi za uongozi, huku benchi la ufundi likikosa mikataba hadi kufikisha mwezi wa nne tangu kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kucheza mechi nane.

“Mtu pekee aliyesaini mkataba ni (hakumtaja), ambaye alishawishi wachezaji kula rushwa ili kupoteza mchezo dhidi ya Majimaji, Februari 2, 2016.

“Mtu huyu alipokea kiasi fulani cha fedha baada ya mchezo huo kumalizika dhidi ya Majimaji,” aliandika Liewig katika waraka wake.

Katika waraka huo, pia kocha huyo alimshutumu msaidizi wake, Bilali Athuman ‘Bilo’ kwa madai ya kushiriki katika vitendo hivyo vya rushwa na kumtaka achunguzwe na taasisi husika nchini.

Suala jingine ambalo lilionekana kumkera Liewig ni juu ya kutolipwa kwa wachezaji wake bonasi zao na malipo mengine ya mkataba waliyoingia na timu hiyo.

Kocha huyo alimshutumu pia mwenyekiti aliyemtaja kwa jina moja la Maeja kwa madai kuwa aliwaahidi wachezaji wote kuwa watalipwa kabla ya mchezo wao dhidi ya Yanga walioshinda kwa bao 1-0.

“Mishahara yao ilitakiwa kuingizwa katika akaunti za wachezaji katika wiki ya kwanza ya Septemba kabla ya mchezo dhidi ya Mbeya City.

“Mwenyekiti aliniomba niwashawishi wachezaji siku mbili kabla ya kucheza mchezo huo bila kulipwa na wangepata haki yao baada ya mchezo, lakini nayo ilikuwa ahadi hewa” ilisema sehemu ya waraka huo.

Mchezo kati ya Mbeya City na Stand ulikuwa na matatizo kwa Liewig, ambaye alichukua uamuzi ulioshindwa kutekelezwa na uongozi.

“Oktoba 4, niliamua kumuengua kocha msaidizi (Bilo) baada ya kugundua kuwa msafara wetu utakuwa na Sir Tiba (kama mkuu wa msafara, Jacob Massawe (nahodha), Kiemba, Muwonge, Revocatus wakiwa kama wasaidizi waliotoa ukweli wa Bilo kula rushwa na kuamua kwa pamoja kumuengua kikosini.

“Lakini, licha ya kuonyesha wasiwasi wangu, hakuna kilichofanyika hata baada ya kuomba kikao, hili lilizuiliwa kwa nguvu kubwa na Sir Mbasha aliyewasiliana na nahodha (Jacob),” uliongeza waraka huo.

Waraka huo umekuja siku chache baada ya kocha huyo kuamua kujiweka kando akidai malipo yake ili kuachana na kikosi hicho cha Stand kinachofanya vizuri katika Ligi Kuu licha ya misukosuko hiyo.

Liewig aliimarisha Stand na kuifanya ishike nafasi ya pili katika msimamo hadi sasa ikiwa nyuma ya Simba kwa pointi tatu.