Kocha wa Azam ageukia Ligi Kuu

Muktasari:

Azam imetolewa na Mbabane Swallos ya Swaziland katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 nyumbani na kuchapwa mabao 3-0 ugenini.

Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Azam, Aristica Cioaba amesema nguvu zao wanazielekeza kwenye Kombe la Shirikisho (FA) na Ligi Kuu Bara ili kuhakikisha wanapata nafasi nyingine ya kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani.
Azam imetolewa na Mbabane Swallos ya Swaziland katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 nyumbani na kuchapwa mabao 3-0 ugenini.
Cioaba alisema safu ya ushambuliaji iliwaangusha katika mchezo wao na Mbabane licha ya kwamba walifanyiwa fitna  kabla ya mchezo, lakini ameamua kuachana nazo kwani hazitawasaidia chochote kwa sasa.
"Licha ya kwamba tulifanyiwa vurugu kabla ya mchezo, lakini  acha tuyaache yapite, kubwa ni kwamba tulitengeneza nafasi mbili za wazi hatukuzitumia hivyo washambuliaji wangu walituangusha katika mchezo ule."
"Hivi sasa tunaangalia mechi za Ligi Kuu na FA ili kutafuta nafasi ya kushiriki tena mashindano ya kimataifa mwakani hivyo ili tutimize malengo yetu ni kuhakikisha tunakusanya pointi za kutosha zitakazotusaidia kupata nafasi tunayohihitaji,"alisema Cioaba
Cioaba alisema ana kazi ya kuwajenga kisaikolojia wachezaji wake ili kusahau yaliyopita na sasa waelekeze nguvu zao  kwenye ligi na kombe la FA.
   "Tuna mechi na Ndanda kwenye robo fainali ya FA hivyo tunatakiwa kuingia nusu fainali kwa kuhakikisha tunashinda mchezo huo  na kisha fainali kisha tutwae ubingwa."