Messi ataja warithi wa Neymar

Madrid, Hispania. Mshambuliaji Lionel Messi amewataja Paulo Dybala, Angel Di Maria na Ousmane Dembele kuwa ndiyo warithi sahihi wa Neymar endapo atahamia Paris Saint-Germain.

Neymar ameendelea kuhusishwa na kutakiwa na Paris Saint-Germain uhamisho unaokadiliwa kufikia pauni 195milioni.

Kwa mujibu wa Don Balon, nyota huyo wa Argentina amemtaja mshambuliaji Paulo Dybala, Angel Di Maria na Mfaransa Ousmane Dembele.

Dybala amekuwa na msimu mzuri tangu alipotua Juventus ambako amefunga mabao 35 katika misimu miwili aliyocheza na miamba hiyo ya Serie A.

Kiungo huyo mwenye miaka 23, amecheza pamoja na Messi katika kikosi cha Argentina pia kuna uwezekano wawili hao wakacheza pamoja ndani ya Nou Camp.

Nyota mwingine aliyetajwa na Messi katika orodha yake ni Angel Di Maria, japokuwa uhamisho huo uenda ukawa na utata kutokana na kuwa amecheza Real Madrid.

Jina la mwisho lililopendekezwa na Messi ni winga wa Borussia Dortmund, Ousmane Dembele.

Msimu uliopita chipukizi huyo wa miaka 20, alifunga mabao nane na kutegeneza pasi za mwisho 18 katika Ligi ya Mabingwa na Bundesliga.