Mipango ya kocha Mourinho yapanguka

Muktasari:

Mourinho amekuwa akitajwa kuwa atapitisha fagio kwenye kikosi chake ambako baadhi ya nyota huenda wakakumbana na panga hilo.

Manchester, England. Idadi ya wachezaji ambao kocha Jose Mourinho amewapiga bei imefikia tisa badala ya wanne aliopanga awali.

Miongoni mwao ni kiungo mkongwe na nahodha wa Ujerumani, Bastian Schweinsteiger ambaye hajaonekana mazoezini Manchester United, ingawa Juan Mata aliyeuzwa na Mourinho zama hizo akiwa Chelsea, amenusurika.

Mourinho amekuwa akitajwa kuwa atapitisha fagio kwenye kikosi chake ambako baadhi ya nyota huenda wakakumbana na panga hilo.

Schweinsteiger alikosekana kwenye mazoezi juzi, huku uvumi ukiendelea kuwa ni miongoni mwa nyota watakaoondolewa kikosini msimu ujao.

Mkongwe huyo ameathiriwa kwa kiasi kikubwa na maumivu akiwa Manchester United msimu uliopita.

Kiungo huyo wa zamani wa Bayern Munich alicheza mechi 13 pekee za Ligi Kuu msimu uliopita, ukiwa mwaka wake wa kwanza kwenye klabu hiyo ya Old Trafford, jambo linaloongeza uwezekano wa kuachwa na Mourinho.