Schweinsteiger aonywa kuhusu Man United

Bastian Schweinsteiger na mkewe Ana Ivanovic

Muktasari:

Gazeti la Sportsmail liligundua kundi la wachezaji wakongwe wa Old Trafford waliochoshwa na kuona picha za mwenzao akimwangalia mkewe, Ana Ivanovic wakati timu ikimaliza msimu katika nafasi ya tano huku Schweinsteiger ‘akila bata’

Manchester, England. Wachezaji wa Manchester United wamemwambia Bastian Schweinsteiger aache mara moja kuangalia tenisi na badala yake afanye mazoezi wakati Mjerumani huyo alipoumia msimu uliopita.

Gazeti la Sportsmail liligundua kundi la wachezaji wakongwe wa Old Trafford waliochoshwa na kuona picha za mwenzao akimwangalia mkewe, Ana Ivanovic wakati timu ikimaliza msimu katika nafasi ya tano huku Schweinsteiger ‘akila bata’.

Schweinsteiger aliambiwa bila kutajiwa majina kuwa wachezaji wenzake wamechoka kumwona akifurahia maisha wakati wakiwa katika wakati mgumu kuiinua Manchester United.

Kiungo huyo wa miaka 32 aliambiwa picha yake akimshangilia mcheza tenisi huyo wa Serbia, Ivanovic mjini Miami na Madrid wakati Manchester United wakisaka nafasi ya nne ilikuwa na ujumbe usiofaa kwa nyota wadogo wa klabu hiyo.

Picha hiyo pia ilimgusa kocha wa Manchester United, Jose Mourinho, ambaye aliamua kwamba Schweinsteiger hana mpango na klabu hiyo kabla hata hajasaini kuinoa miamba hiyo.

Mchezaji huyo wa zamani wa Bayern Munich alicheza katika mechi 13 pekee msimu uliopita na sasa akiozea benchi na kutupwa katika kikosi cha vijana chini ya miaka 23.

Schweinsteiger alivunja ukimya na kuiambia klabu hiyo kupitia akaunti yake ya Twitter anajiandaa kujitoa katika mkataba wake uliobaki wa miaka miwili wa kuitumikia Old Trafford.

Inasadikiwa kwamba Mjerumani huyo ataondoka kabla ya mwishoni mwa mwezi huu, lakini alisisitiza kwamba hatajiunga na timu nyingine ya Ulaya.