Simba : Tumefuata taratibu zote kumsajili Mavugo

Muktasari:

  • Rais wa Vital’O, Benjamin Bikorimana amesema Mavugo bado ana mkataba wa mwaka mmoja na klabu hiyo, hivyo taarifa kuwa amemaliza mkataba siyo za kweli.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba, Zacharia Hanspoppe amesema hawatamuachia Laudit Mavugo hata kama klabu ya Vital’O ya Burundi  inasema bado ina mkataba naye kwani wamefuata taratibu zote kwenye usajili wake.

Rais wa Vital’O, Benjamin Bikorimana amesema Mavugo bado ana mkataba wa mwaka mmoja na klabu hiyo, hivyo taarifa kuwa amemaliza mkataba siyo za kweli.

 “Simba wanapoteza muda na wanajisumbua kwani Mavugo bado tuna mkataba naye, ITC (hati ya uhamisho wake wa kimataifa) yake ipo kwetu, huyu ni mchezaji wetu,” amesema Bikorimana.

Hanspoppe amesema kwa kiwango alichokionyesha Mavugo kwenye tamasha la ‘Simba Day’, Jumatatu iliyopita hawatakubali kumwachia na watapambana hadi haki yao ipatikane

Hata hivyo, Hanspoppe amesema uongozi wa Vital’O una matatizo na watahakikisha wanakwenda hadi Fifa (Shirikisho la Soka la Kimataifa) katika suala hilo.

“Sisi tunachojua Mavugo kamaliza mkataba, ila baadhi ya viongozi wa Vital’O wana matatizo nasi kwani mara ya kwanza tulipotaka kumchukua Mavugo walisema bado ana mkataba wa miaka miwili, tukamuacha hadi amalize ndipo tumchukue.

“Sasa hivi wanaibuka, wanasema ana mkataba wa mwaka mmoja, sasa hatuwaelewi na huwa wana matatizo tangu kipindi kile tunamchukua Tambwe (Amissi), mambo yao yako hivyo hivyo.

“Wakigoma kutoa ITC tunakwenda Fifa kulalamikia hili, nadhani huko ndipo haki itapatikana.

“Tunashangaa kwa nini wenzetu wanaficha mikataba ya wachezaji, tukitaka kumchukua mchezaji tukiwaambia tuonyeshe mkataba wake umebaki muda gani hawasemi, hivyo wanaonyesha ni watu wa shari,” amesema Hanspoppe.

Awali, Simba ilishindwa jaribio lake la kumsajili mshambuliaji huyo na sasa imefanikiwa kunasa saini yake, lakini tayari Vital’O  inadai -usajili wake ni batili.