Simbu: Miguu ilinigomea Rio

Mwanariadha wa Tanzania, Alphonce Simbu akiwa na mtoto wake baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam akitokea Rio de Janeiro, Brazil alikoshiriki Michezo wa Olimpiki na kumaliza katika nafasi ya tano. Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Katika michezo hiyo ya Rio 2016, Simbu alimaliza katika nafasi ya tano akitumia muda wa 2:11:15 katika mbio za Marathon za kilomita 42, akiachwa kwa dakika 2:71 na bingwa Eliud Kipchoge kutoka Kenya.

Dar es Salaam. Mwanariadha shujaa wa Tanzania kwenye Olimpiki mwaka huu, Alphonce Simbu amesema kilichosababisha ashindwe kutwaa medali ni baada ya kuishiwa pumzi alipokimbia kilomita 35.

Katika michezo hiyo ya Rio 2016, Simbu alimaliza katika nafasi ya tano akitumia muda wa 2:11:15 katika mbio za Marathon za kilomita 42, akiachwa kwa dakika 2:71 na bingwa Eliud Kipchoge kutoka Kenya.

“Nilikwenda sanjari na Kipchoge, hadi kilometa 35 na tulikuwa tunachuana sisi wawili.

“Kuna wakati aliniacha, lakini baadaye nikampita, waliokuwa nyuma yetu walikuwa wanapambana ili kutufikia, nilijihisi pumzi zinakata. Nikapunguza mwendo, ndipo aliponiacha,” alisimulia Simbu muda mfupi baada ya kurejea nchini jana akitokea Rio de Janeiro, Brazil.

“Haikuwa kazi rahisi kumaliza wa tano, ushindani ulikuwa mkali, tulikuwa wanariadha zaidi ya 100 kila mmoja alipigania nchi yake, huu ni wakati wetu kujipanga sawa sawa tunaweza,” alisema Simbu.

Simbu aliyeongozana na wanariadha wenzake, Said Makula na Fabiano Joseph alipokewa na wadau mbalimbali wa michezo, akiwamo, Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo (BMT), Mohamed Kiganja na katibu mkuu wa Kamati ya Olimpiki (TOC), Filbert Bayi.