Tanzania yatoka kapa Mbio za nyika za Dunia

Muktasari:

  • Katika mbio hizo wanariadha wa Kenya, Uganda, Uturuki na Ethiopia walitawala na kunyakuwa medali zote, huku Watanzania wakiwa wasindikizaji.
  • Nafasi ya juu iliyopata Tanzania katika mbio hizo iliambualia nafasi ya nane katika mbio za kupokezana vijiti za kilomita nane.

Dar es Salaam.Wanariadha wa Tanzania wameshindwa kwenye mashindano ya mbio za nyika za dunia zilizofanyika kwenye Uwanja wa Kololo, Kampala, Uganda.

Katika mbio hizo wanariadha wa Kenya, Uganda, Uturuki na Ethiopia walitawala na kunyakuwa medali zote, huku Watanzania wakiwa wasindikizaji.

Nafasi ya juu iliyopata Tanzania katika mbio hizo iliambualia nafasi ya nane katika mbio za kupokezana vijiti za kilomita nane.

Wanariadha Faraja Lazaro, Marco Monko, Sicilia Panga na Jackline Sakilu walitumia dakika 24:13 kumaliza mbio hizo, matokeo ambayo hayakuwasaidia kuchukua chochote.

Timu hiyo ilianza kupoteza matumaini ya medali ikiwa nchini kufuatia safari yao kuingiwa na kusubirishwa zaidi ya saa saba, pia ilisafiri zaidi ya saa 30 njiani kwa basi la jeshi ikiwa ni siku mbili kabla ya kuanza mashindano.