Ulimwengu aiacha TP Mazembe

Muktasari:

  • 130: Ni mechi alizocheza Ulimwengu kwa miaka mitano aliyokuwa TP Mazembe.
  • 35: Idadi ya mabao aliyofunga Ulimwengu akiwa na TP Mazembe.

Dar es Salaam. Wakati wachezaji wengi  Tanzania wakiwa na ndoto za siku moja kuichezea TP Mazembe ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC), mshambuliaji Thomas Ulimwengu ametangaza kuachana na klabu hiyo baada ya kuitumikia kwa miaka mitano.

Ulimwengu alijiunga na timu hiyo mwaka 2011 akitokea AFC Academy ya Stockholm, Sweden tangu wakati huo ameichezea klabu hiyo mechi 130 na kufunga mabao 35 katika mashindano mbalimbali na kujijengea sifa kubwa.

Katika taarifa yake kwa mashabiki na viongozi wa timu hiyo, Ulimwengu aliwashukuru kwa kumuunga mkono katika kipindi aliyoitumikia klabu hiyo.

“Katika miaka mitano, Mazembe imeniwezesha kukua na ninataka kuwashukuru viongozi hasa Katumbi (Moise) na mashabiki kwa kuniunga mkono na kuniwezesha kushinda mataji,” alisema Ulimwengu.

Kocha mkuu wa Mazembe, Herbet Velud alisema Ulimwengu alikuwa mchezaji muhimu na kuondoka kwake ni pigo kwa mabingwa hao mara tano wa Afrika.

“Amekuwa hapa na kucheza kwa kiwango cha juu, kuondoka kwake ni masikitiko, lakini tunamtakia kila la kheri katika changamoto mpya.”

Mchezaji huyo alishatangaza kuwa ataondoka katika timu hiyo baada ya mkataba wake kumalizika ili apate fursa ya kucheza soka barani Ulaya.

Katika miaka mitano aliyocheza Mazembe, Ulimwengu alishinda mataji mbalimbali, likiwamo la Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2015.