Wadai Yanga, Azam, Simba zinabebwa

Muktasari:

  • Timu hizo zimedai kuwa ratiba hiyo inatengeneza mazingira rafiki kwa timu hizo tatu kubwa kucheza mechi mfululizo bila kuwachosha wachezaji wao tofauti na timu ndogo, ambazo wamedai zinakomolewa.

Dar es Salaam. Baadhi ya makocha wa klabu za Ligi Kuu Bara wamelilalamikia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu nchini (TPLB) kuzipendelea Simba, Yanga na Azam katika upangaji wa ratiba ya ligi hiyo.

Timu hizo zimedai kuwa ratiba hiyo inatengeneza mazingira rafiki kwa timu hizo tatu kubwa kucheza mechi mfululizo bila kuwachosha wachezaji wao tofauti na timu ndogo, ambazo wamedai zinakomolewa.

Kocha wa Toto African, Rogasian Kaijage alisema: “Tumetoka Mbeya kucheza na Prisons, tukaja Dar es Salaam kucheza na Africana Lyon. Tumefika hapa, mchezo wetu uliokuwa ufanyike Septemba 18 ukasogezwa hadi Septemba 20.

“Sasa hapo tunapata wapi fedha ya kuendelea kuiweka timu kambini? Timu ndogo unaweza ukacheza Mbeya mechi moja halafu unakwenda Dar es Salaam, ukitoka hapo ina kubidi kurudi tena Mbeya kucheza na Mbeya City, hapo haki ipo wapi?” alihoji Kaijage

“Wakati Azam imeenda Mbeya imecheza mechi zote dhidi ya Prisons na Mbeya City, Yanga imekwenda Shinyanga inamaliza mechi zote dhidi ya Mwadui na Stand,” alisema.

Kocha wa Prisons, Abdul Mingange alisema hali hiyo inachangiwa na nguvu ya timu hizo tatu kuwa na viongozi ndani ya shirikisho. “Unajua mchezo wa mpira ni lazima uendeshwe kwa haki ili uweze kupiga hatua,” alisema.

Simba na Yanga zimekuwa zikipewa kipaumbele mno kiasi ambacho zinaweza hata kugomea ratiba ya mechi na zikasikilizwa.

“Kama tunataka soka letu liende mbele, ni lazima ratiba yetu iwe rafiki kwa kila timu badala ya kuzibeba timu fulani na kuzikandamiza nyingine,” alisema Mingange.

Kocha wa Mwadui, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ alisema: “Kila wakati tumekuwa tukipigia kelele suala la kuzibeba hizo timu kongwe, lakini mwisho wa siku matatizo yale yale yanajirudia. “Itafika kipindi, bora tuwaachie ligi wacheze wao wenyewe na hizo timu zao.”

Kocha wa Majimaji, Peter Mhina alisema wanapata wakati mgumu kutokana na ratiba kuwachosha, lakini inabidi wakomae hivyo hivyo kwani lazima ligi ichezwe.

Ikijibu malalamiko hayo, TPLB imezitaka timu zote zinazolalamika kufuata utaratibu unaotakiwa.

Ofisa wa Ligi, Joel Balisidya alisema bodi haiwezi kufanyia kazi malalamiko yanayotolewa kwenye vyombo vya habari. “Hizo timu zote zinafahamu utaratibu ulivyo.

Kama wanahisi hawatendewi haki basi watuletee mezani badala ya kulalamika huko ambako si mahali sahihi,” alisema Balisidya.

Timu iliyoonja joto la ratiba ni JKT Ruvu ambayo ilikuwa Shinyanga kucheza na Stand United huku ikitakiwa kucheza na Mbeya City kwenye Uwanja wa Mabatini Mlandizi.

Baada ya hapo, imepangwa kurejea tena Kanda ya Ziwa, Mwanza kuikabili Mbao FC.