Watano waibeba Yanga ikiichapa Ngaya 5-1

Muktasari:

Mabingwa hao wa Tanzania Bara walifunga mabao hayo kwenye mchezo uliofanyika katika Uwanja wa Moroni na kuifanya kutoka kifua mbele kwa jumla ya mabao 5-1.

Moroni, Comoro. Mabao matano yaliyofungwa na nyota watano wa Yanga; Justine Zullu, Simon Msuva, Obrey Chirwa, Amissi Tambwe na Thaban Kamusoko dhidi ya Ngaya FC ya Comoro yameiwezesha kutoa onyo kwa timu zingine itakazokutana nazo kwenye Ligi ya Mabingwa barani Afrika.

 

Mabingwa hao wa Tanzania Bara walifunga mabao hayo kwenye mchezo uliofanyika katika Uwanja wa Moroni na kuifanya kutoka kifua mbele kwa jumla ya mabao 5-1.

 

Ushindi huo unaifanya Yanga kuweka rekodi ya kuzifunga timu nne za Comoro jumla mabao 36-5  katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Alianza kiungo Mzambia, Zullu kuifunga bao lake la kwanza tangu alipojiunga katika dakika 43 na dakika mbili baadaye Msuva akaifunga bao la pili.

 

Nyota mwingine wa timu hiyo Chirwa akapachika bao la tatu dakika 59 kisha Tambwe akaongeza la nne kabla ya Mzimbabwe Kamusoko kupachika bao la tano katika dakika 73. Wenyeji Ngaya walipata bao la kufutia machozi dakika ya 66 lililofungwa na Said Anfane Boura.

Kabla ya hatua ya makundi, mabingwa hao wa Bara watacheza na mshindi kati ya Zanaco ya Zambia na APR ya Rwanda itaanzia ugenini Machi 16.

 

Zanaco na APR katika mchezo wao wa kwanza uliofanyika jijini Lusaka Jumamosi ulimalizika kwa suluhu na zitarudiana Jumamosi jijini Kigali.