Friday, July 21, 2017

Wayne Rooney alivyoisimamisha Tanzania

 

By Charles Abel, Mwananchi cabel@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Licha ya kuondoka nchini tangu Alhamisi iliyopita usiku, mshambuliaji Wayne Rooney wa Everton, ameandika rekodi sita ambazo huenda zikachukua muda kufikiwa au kuvunjwa na wanasoka wengine kwa muda mrefu.

Mshambuliaji huyo alikuwa sehemu ya msafara wa Everton uliokuwepo nchini kuanzia Jumatano hadi Alhamisi kwa ajili ya kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, ambao uliandaliwa na kampuni ya michezo ya kubahatisha ya SportPesa.

Pamoja na msafara huo wa Everton kujumuisha baadhi ya mastaa wanaotamba kwenye kikosi chake kama nahodha Leighton Baines, Morgan Schneiderlin na Aaron Lennon, ni Rooney pekee ambaye uwepo wake ulifunika ziara ya timu hiyo kutokana na jinsi alivyoteka hisia za mashabiki pamoja na waandishi wa habari.

Bao la kwanza Everton

Katika mechi hiyo dhidi ya Gor Mahia, Rooney alifunga moja kati ya mabao mawili, ambayo Everton iliyapata na kumfanya aweke rekodi ya kuifungia timu hiyo bao katika mchezo wake wa kwanza kuichezea tangu aliposajiliwa rasmi Julai 6 mwaka huu akitokea Manchester United.

Ulinzi mkali

Rooney ndiye mtu pekee katika msafara huo wa Everton aliyewekewa ulinzi mkali kuanzia siku ya kwanza alipowasili hadi wakati wa kuondoka tofauti na wachezaji wenzake.

Mbali na ulinzi wa Jeshi la Polisi, Rooney pia aliandaliwa walinzi maalumu (mabaunsa), ambao kila wakati walikuwa jirani na mchezaji huyo kuhakikisha watu hawamkaribii pindi alipokuwa akienda maeneo tofauti ikiwamo uwanjani.

Avunja rekodi ya Kaka

Ni jambo geni na la kushangaza kuona shabiki wa soka anaingia uwanjani kwa lengo la kumkumbatia mchezaji hasa katika mechi zinazochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Iliwahi kutokea kwa mshambuliaji wa Brazil, Ricardo Kaka, pindi walipocheza na Taifa Stars na Brazil kuibuka na ushindi wa mabao 5-1, wakati shabiki alipomkimbilia Kaka na kumkumbatia.

Baada ya miaka minane kupita bila rekodi kama hiyo kuwekwa, Rooney aliivunja juzi baada ya shabiki aliyevaa jezi ya Manchester United, kuwapenya walinzi na kwenda alipokuwa mshambuliaji huyo na kumkumbatia ingawa muda mfupi baadaye polisi walikwenda kumtoa.

Bao lawapiku Waingereza

Kabla ya Everton kuja nchini, hakuna mchezaji yeyote raia wa Uingereza aliyewahi kucheza na kufunga bao kwenye Uwanja wa Taifa jijini.

Hata hivyo, kupitia bao lake alilowafunga Gor Mahia, Rooney ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza na nahodha wa England kufunga bao katika uwanja huo.

Mchezaji ghali zaidi

Katika msafara wa Everton uliokuja nchini, Rooney ndiye mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kulinganisha na wengine licha ya mshahara huo kupunguzwa kwa zaidi ya asilimia 50 ili ajiunge na timu hiyo.

Ndani ya Everton, Rooney kwa wiki anapokea mshahara wa Pauni 150,000 (zaidi ya Sh300 milioni) kwa wiki.

Mshahara huo pia unaongezwa na Pauni 150,000 kutoka Man United kutokana na mkataba ambao aliingia mwaka jana wa miaka mitano kubaki Old Trafford.

Amaliza kiu ya siku 4,833

Tangu Rooney alipoifungia Everton bao lake la mwisho Machi 13, 2004, mchezaji huyo aliihama klabu hiyo na kutimkia Manchester United, ambako alidumu kwa miaka 13 na miezi miwili na siku 24.

Kwa kuichezea na kuifungia Everton dhidi ya Gor Mahia, Rooney alikata kiu ya siku 4,833 bila kuonekana na jezi ya Everton katika mashindano.

-->