Wazee Simba, uongozi ‘walianzisha’

Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini wa Simba, Mzee Hamisi Kilomoni (kulia) akizungumza na wandishi wa habari kuhusu kutotambua kuitishwa kwa mkutano wa dharula wa timu hiyo jijini Dar es Salasam jana. Kushoto ni Katibu wa Baraza la Waasisi wa Simba, Malik Snous. Picha na Said Khamis

Muktasari:

Baraza hilo limesema mkutano huo ni batili kwa kuwa haujafuata Katiba ya klabu hiyo.

Dar es Salaam. Siku nane kabla ya Simba kufanya mkutano mkuu wa dharura wenye lengo la kujadili marekebisho ya Katiba ya klabu hiyo, Baraza la wadhamini limeibuka na kusema ni batili.

Baraza hilo limesema mkutano huo ni batili kwa kuwa haujafuata Katiba ya klabu hiyo.

Uongozi wa klabu hiyo umeitisha mkutano huo kwa lengo la kujadili mabadiliko ya Katiba ambayo yangetoa nafasi kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji kuwekeza katika klabu hiyo.

Hatua ya kuitishwa kwa mkutano huo wa mabadiliko ni baada ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuzitaka Simba na Yanga kufanyia mabadiliko Katiba zao kabla ya kuingia kwenye michakato mipya.

Itakumbukwa Oktoba 27 mwaka huu, Katibu Mkuu wa BMT, Mohamed Kiganja alisema kuwa timu yoyote hairuhusiwi kubadili mfumo kutoka wanachama kwenda umiliki wa hisa au ukodishwaji hadi marekebisho ya Katiba yatakapofanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria za BMT na kanuni za msajili namba 442 kanuni ya 11 kifungu kidogo cha (1-9) yatakapofanyika.

Kiganja alisema mabadiliko yaliyokuwa yakiendelea kwenye klabu hizo tayari yalikwisha ingia dosari baada ya baadhi ya wanachama kwenda mahakamani kupinga michakato hiyo, pia kupeleka malalamiko Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na BMT kitu ambacho si ishara nzuri endapo yataachwa yaendelee.

 

Baraza la Wadhamini

Mwenyekiti wa baraza la wadhamini wa klabu hiyo ambalo kikatiba ni wasimamizi wa mali za Simba, Hamis Kilomoni alisema baraza hilo limeamua kutoka na kuzungumzia jambo hilo baada ya kupata barua za malalamiko kutoka kwa wanachama waliodai hawakubaliani na mkutano huo ulioitishwa kubadilisha Katiba kutokana na mazingira yaliyojitokeza katika mkutano wa kwanza.

Kilomoni alibainisha baraza hilo linalotambuliwa na msajili wa vyama vya michezo na kuundwa na watu wanne, akiwamo Ramesh Patel, Abdul Wahab Abbas limepitia malalamiko hayo na kubaini wanachama wana sababu za msingi.

“Tumebaini mambo mawili kupitia malalamiko ya wanachama, jambo la kubadili Katiba limewagawa wanachama na kupandikiza chuki miongoni mwao kiasi cha kufikia hatua kupigana na kutozikana na pili wanachama hawajaelimishwa vya kutosha kuhusu mfumo huu.

“Haya mambo yanahitaji kuzingatia Katiba na sheria na sisi (Baraza la Wadhamini) ndiyo tunaosimamia mali za klabu, ndiyo maana tumetoka kuzungumzia.

“Klabu ya Simba inasifika kwa mafanikio tofauti na klabu nyingine,” alisema Kilomoni ambaye katika mkutano na waandishi wa habari aliongozana na Katibu wa Baraza la Wazee, Maliki Abubakar na mjumbe wa baraza hilo, Hassan Abdallah.

Baraza hilo la wadhamini limemuomba mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam kusimamisha mkutano uliopangwa kufanyika Desemba 11 kwa kuwa kuna kila dalili za uvunjifu wa amani kutokana na migawanyiko baina ya wanachama na migawanyiko iliyopandikizwa katika mkutano wa Julai 31, mwaka huu.

“Mkutano uahirishwe hadi uhakiki wa wanachama utakapofanyika, itolewe elimu kwa wanachama wa klabu ya Simba katika matawi yote nchi nzima, lakini kubwa tunamuomba RC Makonda asimamishe mkutano huo kwa ajili ya usalama wa nchi.

“Nyinyi wenyewe mliona rais (Aveva) alitolewa ukumbini kwa ulinzi wa askari katika mkutano uliopita, ni lazima tukae chini, sisi Baraza la Wadhamini tunaamini huo mkutano ni batili,” alisisitiza Kilomoni.

 

Kaburu afunguka

Akizungumzia hilo, Makamu wa rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ amepinga hatua hiyo ya baraza hilo akisema hawana mamlaka ya kuwazuia kuitisha mkutano kikatiba.

“Baraza la wadhamini halina mamlaka ya kuzuia mkutano mkuu, we angalia Katiba ya Simba Ibara ya 20 na 22, mkutano mkuu wa kawaida unaitishwa na Rais kwa kushirikiana na kamati ya utendaji,” alisema Kaburu.

 

Fedha za Okwi, Samatta

Katika hatua nyingine; baraza hilo limeitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza ili kubaini ukweli juu ya fedha za kuwauza Emmanuel Okwi na Mbwana Samatta.

“Rage aliliibua pale katikati ndiyo likasikika, lakini sasa hatujui fedha ziko wapi za Emmanuel Okwi na Mbwana Samatta na inabidi zihifadhiwe kwenye akaunti ya Simba …tunaiomba Takukuru itusaidie kujua fedha ziko wapi maana zile ni mali ya klabu ya Simba, baraza la wadhamini tungependa tujue,” alisema.

Ismail Aden Rage aliwahi kuwa mwenyekiti wa Simba.