Yanga, Kiluvya patamu

Muktasari:

Mchezo huo ni wa kiporo wa hatua ya 16 ya mashindano hayo ambayo bingwa wake ataiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kombe la Shirikisho Afrika na mshindi wake ataungana na timu nyingine saba ambazo zimetinga hatua ya robo fainali.

Dar es Salaam. Utimamu na maandalizi mazuri kisaikolojia ndio jambo pekee litakaloamua matokeo ya mechi ya kombe la FA la 'Azam Sports Federation Cup' itakayofanyika kwenye uwanja wa Taifa kesho kati ya Yanga na Kiluvya United.

Mchezo huo ni wa kiporo wa hatua ya 16 ya mashindano hayo ambayo bingwa wake ataiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kombe la Shirikisho Afrika na mshindi wake ataungana na timu nyingine saba ambazo zimetinga hatua ya robo fainali.

Ingawa inaonekana ni mechi nyepesi kwa Yanga kutokana na kikosi chake kuundwa na wachezaji wenye majina na uwezo mkubwa, mabingwa hao watetezi wa kombe hilo wanapaswa kuingia kwa tahadhali kubwa mbele ya Kiluvya United inayosifika kwa kucheza soka la pasi.

Ni wazi kuwa Yanga inapitia kwenye kipindi kigumu kwa sasa kutokana na matatizo ya kifedha yanayoikabili pamoja na kusumbuliwa na tatizo la majeruhi, hivyo iwapo benchi la ufundi lisipojipanga na kuwaweka saa kisaikolojia wacheaji, wanaweza kuwapa faida Kiluvya kwenye mchezo huo.

Kocha mkuu wa Kiluvya United, Yahaya Issah amesema kuwa mchezo dhidi ya Yanga ni vita ngumu ambayo wanahitaji kuwa sawa kimwili na kiakili ili kuishinda.

"Tunafahamu kuwa Yanga wana matatizo ya nje ya uwanja pamoja na majeruhi lakini mchezo wa mpira siku zote hauamuliwi na vitu kama hivyo zaidi ya uwezo wa uwanjani. Hata Yanga wasipotumia kikosi cha kwanza bado mechi itakuwa ngumu kutokana na ubora wa kikosi chao na tunawaheshimu kwa hilo," alisema Issah.

Kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi amesema kwa kifupi kuwa mipango yao ni kuibuka na ushindi.

"Siku zote mkakati wetu ni kupata ushindi kwenye mechi iliyo mbele yetu pasipo kuangalia tunacheza na nani. Tumejiandaa vyema kuhakikisha tunapata ushindi ili tuvuke kwenda hatua inayofuata," amesema Mwambusi.