Yanga yaitumia salamu Simba

Muktasari:

Yafungua msimu kwa ushindi wa 3-0 dhidi ya Lyon.

Dar es Salaam/Mwanza. Baada ya kufanya vibaya kwenye michezo ya kimataifa ilikotolewa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga imerejea Ligi Kuu na kuanza utetezi kwa kishindo huku Mbeya City ikifufukia ugenini Mwanza.

Ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya African Lyon iliyorejea Ligi Kuu msimu huu ni salamu kwa watani zao, Yanga walioanza kwa ushindi wa mabao 3-1 kabla ya juzi kubanwa na JKT Ruvu na kutoka sare.

Hata hivyo, Yanga ambayo iliandika mabao yake kupitia kwa Deus Kaseke, Simon Msuva na Juma Mahadhi, itasubiri kwa muda kabla ya kukutana na Simba, Oktoba Mosi kwenye ligi hiyo.

Mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga ilionyesha kiwango kizuri dhidi ya Lyon iliyoonyesha ugeni.

Udhaifu wa safu ya ulinzi ya Lyon kujaribu kuwatengenezea washambuliaji wa Yanga mitego ya kuotea, ilianza kuonekana tangu dakika ya nane ya mchezo baada ya Amissi Tambwe kukosa bao la kwa kichwa alichopiga akiunganisha krosi ya Haruna Niyonzima kutoka nje.

Ujanja wa washambuliaji wa Yanga uliwasaidia. Dakika ya 18, Kaseke aliwapatia bao la kuongoza kutokana na kumhadaa kipa Youthe Rostand baada ya kupokea pasi ya Msuva.

Awali, Yanga waligongeana pasi fupi na Msuva alipiga pasi ya kupenyeza kwa Kaseke ambaye wachezaji wa Lyon walidhani alikuwa ameotea.

Licha ya kufungwa bao hilo, Lyon walionyesha utulivu hasa kwenye safu yao ya kiungo iliyongozwa na Musa Nampaka. Dakika ya 25, Hamad Tajiri alimuangusha Tambwe, lakini mwamuzi Rajab Mrope kutoka Ruvuma aliamuru mpira uelekezwe langoni mwa Yanga.Hali ya unyevunyevu kwenye uwanja ilionekana kuiathiri zaidi Yanga ambayo mara nyingi pasi zao zilinaswa na wapinzani wao, Lyon.

Kipindi cha pili, Yanga ilionekana kunufaika zaidi na mabadiliko yaliyofanywa baada ya Lyon kumtoa Amani Peter na kumuingiza Awadh Juma.

Mabadiliko hayo yaliisaidia Yanga kutawala kiungo na haikushangaza kuona dakika ya 59, Msuva akiipatia timu hiyo bao la pili kwa kumpiga chenga kipa wa Lyon baada ya pokea pasi kutoka ya Thabani Kamusoko.

Dakika ya 73, Lyon iliwatoa, Musa Nampaka na Omary Abdallah na nafasi zao kuchukuliwa na Ramadhan Kipalamoto na Abdul Hilal.

Msuva aliyekuwa mwiba kwa mabeki wa Lyon, alitolewa dakika ya 76 na nafasi yake kuchukuliwa na Mahadhi aliyeipa timu yake bao la dakika za majeruhi.

Hata hivyo, tatizo la majeruhi liliendelea kuitesa Yanga kwani katika mchezo huo ilikuwa na wachezaji sita kwenye benchi lake badala ya saba kama ilivyozoeleka.

Dakika ya 88, Yanga ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Donald Ngoma na kumuingiza Matheo Anthony.

 

Vikosi jana Yanga

Deogratius Munishi, Hassan Ramadhan ‘Kessy’, Mwinji Haji, Andrew Vincent, Vincent Bossou, Thabani kamusoko, Simon Msuva/Juma Mahadhi, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma/Matteo Anthony, Amissi Tambwe, Deus Kaseke.


African Lyon

Youthe Rostand, Bakari Jaffari, Halfan Twenye, Hamad Tajiri, William Otong, Omary Salum, Amani Peter, Mussa Nampaka, Tito Okello, Hood Mayanja na Omary Abdallah

 

CCM Kirumba, Mwanza

Kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza wenyeji Toto Africans walikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Mbeya City.

Mbeya City ilipata bao hilo pekee lililofungwa na Haruna Shamte kwa mpira wa adhabu uliokwenda moja kwa moja wavuni na kumwacha kipa wa Toto asijue la kufanya.