Yanga yajifariji hatua iliyofikia

Muktasari:

  • Yanga ilitinga hatua ya makundi ya mashindano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na inaendelea na michezo ya Kundi A lenye timu za TP  Mazembe (DR Congo), MO Bejaia (Algeria) na Medeama ya Ghana.

Takoradi, Ghana. Licha ya Timu ya Yanga kuendelea kufanya vuibaya katika mashindano ya kimataifa msimu huu, imeonekana kupiga hatua kubwa ikilinganishwa na michuano mingine iliyowahi kucheza huko nyuma.

Yanga ilitinga hatua ya makundi ya mashindano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na inaendelea na michezo ya Kundi A lenye timu za TP  Mazembe (DR Congo), MO Bejaia (Algeria) na Medeama ya Ghana.

Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh amesema hatua ambayo timu yake imefika msimu huu, ni mara ya kwanza tangu miaka mingi kupita na wachezaji waliocheza kwa wakati huo wengi wamesha staafu soka.

Saleh amesema kutokana na kuwa na kikosi kilichotinga kwa mara ya kwanza katika hatua ya makundi kikiwa na wachezaji wanaocheza kwa mara ya kwanza michuano mikubwa.

“Yanga iliwahi kuifikia hatua kama hii miaka mingi nyuma, hivyo huwezi kuona mchezaji humu mwenye uzoefu mkubwa na mashindano hayo. Hiyo ni moja ya sababu za kusuasua kwetu, pia katika makundi, japo bado tunacheza vizuri kama timu ambayo msimu uliopita ilicheza kwenye mzunguko,” alisema Saleh.

Meneja huyo aliongeza kuwa bado wanacho kikosi imara kinachoweza kuwa pamoja msimu ujao kwani klabu hiyo  ina nafasi ya kucheza tena kwenye mashindano ya kimataifa mwakja kesho. “Kwa jinsi ilivyo, unaweza kuona tuna mwanzo mzuri wa msimu ujao, hata kocha atakuwa huyu (Hans Pluijm) tunamuamini kwani amesaini nasi juzi mkataba mwingine wa miaka miwili, nadhani tutakuwa tumejua nini cha kuongeza,” alisema.