Mikakati mipya ya kuzalisha sukari

Muktasari:

Deo Lyatto alisema uzalishaji katika viwanda vya ndani umeonyesha mafanikio makubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Morogoro. Kampuni za  sukari nchini  zimedhamiria kuongeza uzalishaji kutoka tani 330,000 kwa mwaka hadi 690,000 ifikapo 2020, ili kutosheleza soko la ndani.

Hayo yalibainishwa kwenye mkutano wa wadau wa sukari, ambao walisema uzalishaji wa  nchini kwa sasa ni tani 330,000 huku mahitaji halisi ya bidhaa hiyo yakiwa tani 455,000 kwa mwaka.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Mfuko wa Maendeleo ya Sukari Tanzania  (SIDTF), Deo Lyatto alisema uzalishaji katika viwanda vya ndani umeonyesha mafanikio makubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Lyatto alisema licha ya sekta hiyokukabiliwa na changamoto mbalimbali, wamedhamiria kufikia uzalishaji wa tani 690,000 kwa mwaka ifikapo 2020.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Miwa Tanzania, Dk George Mlingwa alishukuru Kiwanda cha Kilombero kwa kuongeza bei ya miwa kwa wakulima wa nje toka Sh50,000 hadi 100,000 kwa tani.

Dk Mlingwa alitoa wito kwa viwanda vingine kuongeza bei ya miwa, kwani uandaaji eka moja ya miwa inagharimu siyo chini ya Sh1 milioni moja.

Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Sukari Tanzania (Sudeco), Henry Semwanza alisema bodi imekuwa ikishirikiana na Serikali kuhakikisha viwanda vya ndani vinalindwa ili viendelee kuchangia katika pato la Taifa.

Hivi sasa kuna viwanda vitano vya kuzalisha sukari ni vitano ambavyo ni TPC Moshi, Kagera Sugar, Manyara Sugar, Mtibwa na Kilombero. Pia, vimesaliwa vitatu vya Bagamoyo, Mbigili na Mkulazi vimesajiliwa.