Mikataba ya ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi yasainiwa

Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk Augustine Mahiga ilisema juhudi za kutafuta suluhu zilisimama kutokana na mabadiliko ya uongozi katika nchi hizi mbili.

Muktasari:

Mikataba hiyo imesainiwa baada ya kikao cha Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Tanzania na Malawi, kufanyika kutokana na maelekezo ya marais wa nchi hizo ambao walikutana nchini Ethiopia katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU).

Dar es Salaam. Tanzania na Malawi zimesaini mikataba ya kushirikiana katika mashauriano ya kisiasa, kidiplomasia na usafiri wa anga kwa kusaidia kuweka mazingira mazuri ya kushughulikia mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa.

Mikataba hiyo imesainiwa baada ya kikao cha Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Tanzania na Malawi, kufanyika kutokana na maelekezo ya marais wa nchi hizo ambao walikutana nchini Ethiopia katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU).

Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk Augustine Mahiga ilisema juhudi za kutafuta suluhu zilisimama kutokana na mabadiliko ya uongozi katika nchi hizi mbili.

“Japo Tanzania na Malawi zinatofautiana katika mpaka wa Ziwa Nyasa, lakini tofauti hizo zisiwe kikwazo cha kushirikiana katika maeneo mbalimbali kwa faida ya wananchi,” alisema Dk Mahiga.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Francis Kasaila alisisitiza umuhimu wa kuimarisha miundombinu ili Serikali ya Malawi na wafanyabiashara wasafirishe bidhaa kwa urahisi kutoka jijini Dar es Salaam.