Miradi mikubwa minne yaipa ulaji Tanzania

Mwenyekiti wa CILT, George Makuke akizungumza na waandumishi wa habari. Kushoto ni Katibu Taasisi hiyo, Ramadhan Sawaka.

Muktasari:

Miradi inayoipa Tanzania ulaji huo ni ule wa mabasi ya mwendo wa haraka, usafiri wa treni wa Ubungo-Pugu, ujenzi wa daraja la juu 'fly over' la Tazara na kituo cha daladala cha Simu 2000

Dar es Salaam. Tanzania itakabidhiwa uenyekiti wa Taasisi ya Kimataifa ya Lojistiki na Uchukuzi (CILT) Kanda ya Afrika kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Aprili, 2018 nchini Nageria.

Uenyekiti huo wa Afrika unaipa Tanzania u-makamu wa Rais wa CILT duniani na ujumbe wa kamati ya kimataifa ya uongozi wa taasisi hiyo ambayo mlezi wake ni Malkia Elizabeth wa Uingereza.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo Machi 8, 2018, mwenyekiti wa CILT, George Makuke amesema Tanzania itakabidhiwa uongozi huo Aprili 14- 16 mwaka huu katika mkutano utakaofanyika Abuja, Nageria.

Amesema baadhi ya mambo yaliyoiwezesha Tanzania kupata uenyeji huo ni jitihada zinazofanywa na Serikali katika nyaja za usafiri kwa kipindi cha miaka minne iliyopita.

Ametaja baadhi ya miradi ni ule wa mabasi ya mwendo haraka, usafiri wa treni wa Ubungo-Pugu, ujenzi wa daraja la juu 'fly over' la Tazara na kituo cha daladala cha Simu 2000.

Makuke amesema kupitia uongozi huo Afrika na duniani,  unaipa fursa adhimu ya kuandaa mkutano ifikapo Aprili mwakani utakaofanyika Zanzibar ambao utashirikisha zaidi ya wanachama 5,000 kutoka nchi mbalimbali duniani.

Naye Katibu wa CILT, Ramadhan Sawaka amesema licha ya Tanzania kuwahi kuandaa mkutano huo, "Watanzania hatuchangamkii fursa, zilizopo hivyo tuchangamkie fursa kupitia mkutano ujao."

Amesema kuna uzoefu na mafunzo ambayo Tanzania itayapata kutokana na wajumbe wa mkutano kutembelea miundombinu mbalimbali na kuweza kujifunza jinsi ya kuboresha hapa nchini.