Mitandao ya kijamii inaharibu wanafunzi-sheikh

File Photo

Muktasari:

Sheikh wa Msikiti wa Mshikamano mjini Shinyanga, Msafiri Kitumbo ameitoa rai hiyo katika mahafali ya kidato cha nne ya Jumuiya ya Kiislamu (Tamsya), yaliyojumuisha sekondari 21 za Manispaa ya Shinyanga.

Shinyanga. Wanafunzi wa shule za sekondari wametakiwa kuacha kutumia mitandao ya kijamii kwa mambo ambayo hayawezi kuwajenga kimasomo.

Sheikh wa Msikiti wa Mshikamano mjini Shinyanga, Msafiri Kitumbo ameitoa rai hiyo katika mahafali ya kidato cha nne ya Jumuiya ya Kiislamu (Tamsya), yaliyojumuisha sekondari 21 za Manispaa ya Shinyanga.

Amesema mitandao hiyo ni chanzo cha kuporomoka kwa maadili na kuchangia baadhi ya wanafunzi kufanya vibaya katika masomo yao.

Sheikh Kitumbo amesema wanafunzi hutumia muda mwingi kuangalia picha cha za utupu badala ya kusoma vitabu mbalimbali ili kuongeza maarifa.

“Kuna faida na hasara kwenye kutumia mitandao ya kijamii, lakini wanafunzi wenye akili wanaitumia kuperuzi na kujadili masomo na wenzao, wapo wengine kazi yao ni kutuma picha za ajabu,” amesema Sheikh Kitumbo.

Amesema kati ya wanafunzi 158 wanaohitimu, wasichana ni 91 na wavulana ni 67.

Mwenyekiti wa Tamsya Mkoa wa Shinyanga, Hamis Jabiri ametumia fursa hiyo kuwahimiza wanafunzi hao kuzingatia maadili ya dini yao yatakayowasaidia kuwajengea msingi mzuri wa elimu.

Mwanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Uhuru, Omary Omary amekiri baadhi yao kushuka kitaaluma kutokana na kuitumia vibaya mitandao hiyo ikiwamo Facebook, Twitter, Instagram na WhatsApp.