Mjadala wa utekaji ulivyofunika bajeti ya PM

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akijadiliana jambo na mbunge wa luteuliwa, Abdallah Bulembo walipokuwa katika kikao cha nane cha Bunge la Bajeti mjini Dodoma. Picha ya Maktaba

Muktasari:

Sehemu kubwa ya mjadala wa bajeti hiyo ilitawaliwa na suala hilo lililoshika kasi baada ya msanii wa muziki wa rap, Roma Mkatoliki kutekwa na watu wasiojulikana na baadaye kuachiwa huru. 

Dar es Salaam. Pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusisha taasisi muhimu kama Bunge la Jamhuyri ya Muungano, uratibu wa shughuli za Serikali na maendeleo ya sekta binafsi, hotuba ya bajeti ya mwaka 2017/18 ilitekwa na sakata la utekaji.

Sehemu kubwa ya mjadala wa bajeti hiyo ilitawaliwa na suala hilo lililoshika kasi baada ya msanii wa muziki wa rap, Roma Mkatoliki kutekwa na watu wasiojulikana na baadaye kuachiwa huru.

Kabla ya tukio hilo, mwanamuziki mwingine, Ney wa Mitego alikamatwa na polisi akiwa mkoani Morogoro na kusafirishwa hadi Dar es Salaam, akidaiwa kurekodi wimbo unaoikosoa Serikali, lakini aliachiwa huru baada ya Rais John Magufuli kusema ameupenda wimbo huo unaoitwa “Wapo”.

Baada ya matukio hayo, ofisa mteule wa Rais alivamia studio za kituo cha televisheni cha Clouds Media akiwa na askari wenye silaha kali na siku nne baadaye askari kanzu walimtishia bastola mbunge wa Mtama, Nape Nnauye.

Matukio hayo ndiyo yaliyoamsha mjadala mzito baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kusoma bajeti yake Aprili 6.

Pamoja na taasisi muhimu kuwa chini ya Waziri Mkuu, hotuba ya bajeti pia ilizungumzia masuala ya Serikali kuhamia Dodoma, hali ya siasa nchini na maendeleo ya kisekta kama kilimo na mifugo, madini, viwanda, maliasili na utalii.

Hoja nyingine zilikuwa ni huduma za kiuchumi kama umeme, maji, ardhi, barabara usafiri wa majini, anga na reli na mawasiliano na kwa ujumla ofisi hiyo iliomba kuidhinisha Sh171.66 bilioni, zikiwemo Sh121. 65 bilioni kwa ajili ya Mfuko wa Bunge.

Lakini hayo hayakutikisa kama suala la utekaji na uvamizi, kiasi cha wabunge kuomba chombo hicho kiahirishe shughuli zake ili kulijadili.

Wakati wabunge wa chama tawala, CCM wakiitetea Serikali kila inapobanwa bungeni, suala la utekaji liliunganisha wabunge wote.

Kitendo hicho kilifanya mawaziri ndio wabebe jukumu la kupambana, hasa pale wabunge wa upinzani walipokuwa wakichangia hoja za kuituhumu Serikali.

Wabunge walikuwa sahihi

“Wabunge walikuwa sahihi kuzungumzia suala hilo kwa sababu lina umuhimu wa pekee,” alisema mwenyekiti wa kamati ya uongozi ya CUF, Julius Mtatiro.

“Uzoefu unaonyesha kuwa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu huwa inapita tu hata ikijadiliwa kiasi gani kwa sababu Bunge lile lina wabunge wengi wa CCM. Ndiyo maana wabunge wengi waliona wasipoteze muda kujadili kitu ambacho kitapitishwa tu, wakaona wajikite katika matukio ya utekaji maana ni mambo ya msingi.

“Ni kweli walipindisha mjadala, lakini walikuwa wanajadili masuala ya muhimu. Tungekuwa na Bunge linaloweza kubadili bajeti kweli, kweli wangejikita kwenye mjadala huo.”

Lakini mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Emmanuel Malya alisema wabunge hawakutoka nje ya mada.

“Kazi ya Bunge ni kuisimamia Serikali ili itekeleze sera zake vizuri. Kwa mfano kusimamia utekelezaji wa bajeti ya Serikali, kuwakilisha wananchi na kutunga sheria. Suala la usalama wa wananchi ni la muhimu, lakini wanapaswa pia kujadili mambo yote,” alisema.

“Linapokuja suala lenye maslahi ya Taifa, wabunge hawapaswi kugawanyika bali wanajadili kwa pamoja. Kwa hiyo, kujadili utekaji si kupotoka bali walipaswa kwenda mbali zaidi ya hapo,” alisema Dk Malya.

Lakini katibu mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk Khamis Mwinyimvua anaona wabunge waliamua kulikuza suala hilo.

“Mimi ninachojua bajeti imejadiliwa kwa kina. Hayo mambo ya utekaji yalichukua attention ya wabunge tu, lakini kuna maswali mengine yaliulizwa na kwa kweli watendaji wetu wamefanya kazi kubwa kuyajibu. Kwa hiyo, mimi naona bajeti imepita kwa ushindani kabisa,” alisema.

Alisema kabla ya bajeti kufikishwa bungeni, hujadiliwa katika kamati za bunge.

“Nchi nyingine huwa zikishapitishwa kwenye kamati hazifiki hata bungeni, lakini hapa bado tunapeleka bungeni. Kwa hiyo mimi naona bajeti yetu imetendewa haki kabisa,” alisema Mwinyimvua.

Hoja za wabunge

Wakati wa mjadala wa bajeti hiyo, wabunge waliibua zaidi suala la utekaji pengine kuliko bajeti yenyewe.

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe ndiye aliyezungumza kwa hisia kali na pia kudai kufahamishwa na baadhi ya mawaziri kuwa ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa kuna kikundi ambacho kinahusika na utekaji watu.

Alidai kuna Wabunge kumi na moja ambao wamo kwenye orodha ya kutekwa, akiwemo yeye mwenyewe.

“Hatuwezi kulifumbia macho jambo hili, Watanzania wanatekwa na watu wasiojulikana,” alisema Bashe.

Wakati fulani, Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene alipotaka kumbana mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe athibitishe tuhuma kwamba Idara ya Usalama wa Taifa inahusika na utekaji, Bashe alinyanyuka na kusema yeye ni mmoja kati ya watu waliotekwa na maofisa hao, jambo lililomfanya mwenyekiti wa Bunge siku hiyo amtulize kwa kumweleza kuwa uongozi umechukua suala lake.

Hoja kama hiyo ilitolewa na mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilal (CCM) ambaye alisema anaogopa kufika jijini Dar es Salaam kwa sababu alitishiwa na mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama.

“Nilikuwa sitaki kusema lakini ngoja hili niseme, tena mimi sikutishwa kwa maneno, yeye mwenyewe nilikutana naye uso kwa uso akiniambia, ‘nyie wabunge mmezidi unafiki’,” alisema Hilal.

Kwa bahati mbaya zaidi, maneno haya ameyatamka mbele ya Mkuu wa Wilaya wa Kinondoni (Ally Hapi), akasema ‘Wabunge mmezidi unafiki, na nita-deal na nyie nikianza na wewe’.”

Aeshi alitumia fursa hiyo kulitaarifu Bunge na ndugu zake kuwa wakiona haonekani Dar es Salaam, wajue ni kwa ajili hiyo.

Mjadala wa utekani uliibua hadi suala la kutoweka kwa Ben Saanane, ambaye ni msaidizi wa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Suala hilo liliibuliwa na Zitto

“Taarifa zinatoka chini chini, sio rasmi, kwamba huyu kijana ametoweshwa. Kwamba alishikiliwa na watu wa Idara ya Usalama na amepotezwa,” alisema kiongozi huyo mkuu wa ACT Wazalendo.

“Jeshi la Polisi wana taarifa za mawasiliano ya mwisho ya Ben Saanane kwa kutumia simu yake ya mkononi, ambayo inaonekana ilipoteza mawasiliano akiwa maeneo ya Buguruni siku aliyotekwa tena tangu siku hiyo hapakuwa na mawasiliano tena.

“Watanzania wamesahaulishwa yote haya, Polisi mpaka leo hawajamkamata hata mtu mmoja juu ya yote hayo. Sababu kubwa ni ukimya wetu. Sisi wabunge tumepewa ridhaa na wananchi wenzetu kuyasema haya, tumepewa mamlaka ya kuihoji Serikali kuhusu mambo ya wananchi, na usalama wao na mali zao ni jambo la kwanza la msingi kabisa.”

Wakati mjadala huo ukiendelea, Mbowe alikusudia kutoa shilingi akimtaka Waziri Mkuu kutoa kauli ya kuzuia kile alichodai kuwa ni kikosi maalumu cha utesaji, utekaji udhalilishaji na mauaji, alichosema kinachoratibiwa na Idara ya Usalama wa Taifa, kwa kuwa kikundi kazi hicho kinavunja Katiba na sheria za nchi.

Hoja hiyo iliungwa mkono na Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu aliyesema wapo watu 18 anaowatetea Mahakamani walio tayari kutoa ushahidi wa kikundi hicho kinachodaiwa kutumia nyumba iliyopo Mikocheni na nyingine Oysterbay.

Lissu alidai kuwa baadhi ya watuhumiwa wa makosa ya mitandao na uchochezi wamekuwa wakisafirishwa kutoka mikoani mpaka kwenye nyumba hizo kuteswa kinyama bila jamii kujua.

Hata hivyo, hoja hiyo ilipingwa vikali na Serikali, hasa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), Jenister Mhagama na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Utumishi), Angellah Kairuki.

Walimwomba Waziri Mkuu asitoe kauli yoyote kwa kuwa jambo hilo ni uchochezi, huku pia wakimtaka Spika kutoruhusu mjadala huo.