Mkakati wa kutoa chanjo ya ini kupunguza gharama

“Pia, wizara inaangalia uwezekano wa kupata wadau kwa ajili ya kushirikiana nao katika kazi ya kutoa chanjo hii. Kwa sasa, mtu binafsi anayetaka kujikinga na Hepatitis B inabidi alipie katika sekta binafsi.”

Waziri Ummy Mwalimu 

Muktasari:

Kwa sasa ni watu wachache wanaoweza kumudu

Dar es Salaam. Wakati maambukizi ya homa ya ini yakiongezeka nchini, Serikali imesema ipo katika mikakati kuhakikisha inaanza kutoa chanjo ifikapo 2018/19.

Kufuatia mpango huo, tayari Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto imefanya mchanganuo rasmi ambao unaonyesha kiwango cha gharama ya kununua chanjo na vitendanishi vya vipimo vya awali, kutunza, kusambaza chanjo na shughuli ya uchanjaji.

Akizungumza katika siku ya maadhimisho ya homa ya ini duniani hivi karibuni, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema kwa sasa chanjo zimekuwa zikitolewa kwa watoto wadogo tangu mwaka 2003 na hakuna chanjo inayotolewa kwa watu wazima.

Serikali inahangaika kupata chanjo hiyo wakati kiwango cha maambukizi ya hepatitis b ni asilimia 16, ukilinganisha na cha sasa cha virusi vya Ukimwi ambacho ni asilimia 5.3.

Waziri Ummy alisema mpaka sasa ni sekta binafsi pekee inayotoa chanjo hiyo kwa watu wazima, ambayo inapatikana kwa kati ya Sh50,000 na Sh75,000 kwa mtu mmoja kwa dozi moja.

Akizungumzia suala hilo, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Mohammed Kambi alisema vituo vinavyotoa chanjo hiyo ni Premier Care Clinic, IST na Hindu Mandal kwa Mkoa wa Dar es salaam.

“Ni matarajio yetu kuwa gharama hizi zitapungua kwa kiwango kikubwa na kuwezesha chanjo kupatikana katika vituo vingi vya kutolea tiba hasa vya umma, baada ya uamuzi wa Serikali kununua dawa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji. Bei ya chanjo ya homa ya ini Bohari ya Dawa (MSD) sasa inauzwa Sh5,300 kutoka Sh22,000,” alisema Dk Kambi.

Ukubwa wa tatizo

Waziri Ummy alisema kwa sasa maambukizi ni makubwa mara 10 zaidi ya Virusi Vya Ukimwi  (VVU) na kwamba kati ya watu 100, wanane wanaweza kuwa na maambukizi sugu ya ugonjwa huo na wasionyeshe dalili.

Licha ya mwamko mdogo wa kupima afya, asilimia sita ya Watanzania wamekutwa na maambukizi hayo kupitia huduma ya kuchangia damu, huku ugonjwa huo ukiongoza kwa kuua baada ya maambukizi kufikia asilimia 16.

“Tanzania utafiti na takwimu chache zilizopo zinaonyesha uwepo wa maambukizi ya virusi vya hepatitis B na C. Mfano kati ya wachangiaji damu 200,000  mwaka jana, asilimia sita kati yao takriban 12,000 walikuwa na maambukizi ya hepatitis B,” alisema.

Pia, alisema utafiti unaonyesha kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini, homa ya ini inayosababishwa na virusi vya aina B inakadiriwa kuwapo kwa asilimia 16 hadi 50.

Alisema homa ya ini inayosababishwa na virusi aina ya C,   inakadiriwa kuwapo kwa asilimia mbili miongoni mwa wanajamii.

“Maambukizi ya homa ya ini ya aina ya B na C (Hepatitis B na C) ni tatizo kubwa miongoni mwa watu wenye maambukizi ya virusi vya Ukimwi,” alisema.