Mke wa Dk Mwakyembe kuzikwa keshokutwa

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kulia), akizungumza na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alipokwenda kumpa pole  baada ya kufiwa na mkewe, Linah  Mwakyembe aliyefariki dunia usiku wa kuamkia jana katika  Hospitali ya Aga khan jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

DONDOO

Mwili wa marehemu unasafirishwa  kesho mchana kwenda Songwe, kisha Kyela kwa maziko.

Dar es Salaam. Mwili wa mke wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe unatarajiwa kuzikwa keshokutwa, wilayani Kyela Mkoa wa Mbeya.

Linah Mwakyembe alifariki dunia usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Aga Khan alipokuwa amelazwa kwa matibabu ya saratani ya matiti.

Msemaji wa familia, Solomoni Kivuyo alisema ibada ya maziko itafanyika kesho  mchana katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kunduchi, Dar es Salaam, kisha mwili utapelekwa uwanja wa ndege na kusafirishwa hadi Songwe na baadaye Kyela.

“Tutafanya maziko Jumatano mchana,” alisema  Kivuyo.

 Akizungumzia ugonjwa uliokuwa ukimsumbua marehemu, alisema: “Kwanza alitibiwa Muhimbili (Hospitali ya Taifa-MNH), kisha akapelekwa Aga Khan, baadaye akapelekwa India ambako alitibiwa akapata nafuu na akarejea nyumbani. Baadaye aliugua tena akapelekwa Uturuki ambako alitibiwa na kupata nafuu akarejea nyumbani. Lakini wiki tatu zilizopita, hali yake ilibadilika, akapelekwa Aga Khan na usiku wa kuamkia leo (jana ) akafariki dunia.”

Baadhi ya viongozi wa Serikali waliofika msibani hapo ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye pia aliwasilisha salaam za rambirambi kutoka kwa Rais John Magufuli, ambaye yuko Chato, mkoani Geita.

Wengine ni pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, Waziri wa Kilimo na Mifugo Dk Charles Tizeba, wabunge mbalimbali, Meya wa Kinondoni, Benjamin Sitta na Waziri Mkuu mstaafu Salim Ahmed Salim.