Mo Dewji alivyotikisa ndani na nje ya Tanzania

Muktasari:

Ni kutokana na tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara bilionea kijana zaidi barani Afrika ambalo limetawala mijadala karibu kila kona ya dunia, huku baba akiiachia polisi 


Dar/mikoani. Tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji si tu limezua hofu ya usalama wa raia, ila limetikisa ndani na nje ya nchi.

Mfanyabiashara huyo mwenye utajiri unaokadiriwa kuwa Sh3.5 trilioni alitekwa jana saa 11 asubuhi na watu wasiofahamika katika Hoteli ya Colosseum, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Tukio hilo la mfanyabiashara huyo anayefahamika zaidi kwa jina la Mo limezua hofu maeneo mbalimbali nchini na watu wamekuwa wakijiuliza maswali mengi kuhusu chanzo cha tukio hilo, ambacho bado hakijafahamika.

Habari za kutekwa kwa Dewji (43), zilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii jana saa moja asubuhi, kabla ya kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa saa mbili asubuhi.

Akizungumza na waandishi wa habari hotelini hapo, kamanda huyo alisema Dewji ambaye ni mwekezaji wa klabu ya Simba alifika hotelini hapo kwa lengo la kufanya mazoezi kwenye gym iliyopo hapo na kupatwa na janga hilo.

Mambosasa ambaye aliliambia Mwananchi kuwa wanawashikilia watu 12 kutokana na tukio hilo alisema waliomteka mfanyabiashara huyo ni Wazungu wawili.

“Asubuhi ya leo (jana), Wazungu wawili walikuwa na gari aina ya (Toyota)Surf. Kulikuwa na magari mawili, moja lilikuwa ndani (ya uzio) na jingine nje. Gari la ndani liliwasha taa ghafla na lile lililokuwa nje likaingia na kwenda kupaki karibu na gari la Mo Dewji lililokuwa limepaki,” alisema Mambosasa.

“Wazungu wawili wakatoka na kumbana MO Dewji baada ya kutoka ndani ya gari lake na kisha kumpakia katika gari lao aina ya Surf kisha wakaondoka naye kusikojulikana,” alisema Mambosasa.

Dereva Uber asimulia alivyotekwa

Maelezo hayo yanatofautiana na ya dereva mmoja anayeendesha magari ya kukodisha ya mtandao wa Uber, ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini.

Dereva huyo aliyekuwa anakwenda kumshusha abiria katika hoteli hiyo saa 11 asubuhi alisema, “Tulikuwa tunakaribia eneo hilo, mara mbele yetu tukaona watu wanne wameshuka kwenye gari dogo wakiwa wamejifunika usoni, wakapiga risasi moja juu, wale askari wa hoteli kila mmoja akakimbia.

“Waliingia ndani ya hoteli na kutoka na mtu, ambaye nilimjua kuwa ni Mo,” alisimulia dereva huyo ambaye alidai muda mwingi alikuwa amejiinamia kwenye gari akihofia maisha yake.

Alisema baada ya watu hao kumchukua mfanyabiashara huyo, waliondoka na gari kwa kasi kuelekea maeneo ya Masaki.

Hali ilivyokuwa nyumbani

Nyumbani kwa Dewji maeneo ya Oysterbay, ulinzi uliimarishwa huku ndugu, jamaa na marafiki wakifika na kuondoka katika nyumba ya bilionea huyo.

Sauti za kulia zilisikika kutoka ndani na kadri muda ulivyokuwa ukisogea sehemu ya maegesho ya magari ilikuwa ikijaa kutokana na wingi wa waliofika nyumbani hapo. Baadhi ya ndugu hao waligoma kurekodiwa wakisema ndani kwa Mo hakuna taarifa sahihi za alipo ndugu yao.

Baba yake azungumza

Gulam Dewji Hussein, baba wa Mo alipozungumza na Mwananchi kuhusiana na tukio la kutekwa kwa mtoto wake, alisema hawezi kulitolea maelezo tukio hilo kwa sasa.

“Sina cha kuzungumza, naomba muwatafute polisi wao wanaweza kuwa na maelezo zaidi,” alisema Gulam.

Wanasiasa washtushwa

Wanasiasa mbalimbali nchini walitoa maoni wakionyesha kusikitishwa na tukio hilo.

Zitto Kabwe, January Makamba, Hussein Bashe na Nape Nnauye ambao ni wabunge walitumia mitandao yao ya Twitter kuzungumzia tukio hilo la kutekwa kwa Mo Dewji ambaye amekuwa akitajwa na Jarida la Forbes kuwa miongoni mwa mabilionea vijana Afrika.

Makamba, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ameandika, “Nimezungumza na baba yake Mohammed Dewji. Habari za kutekwa kwa rafiki yetu Mo ni za kweli. Nimesikitishwa sana. Naamini polisi watatoa taarifa kamili. Mohammed ana familia na watoto wadogo.”

Mbunge huyo wa Bumbuli amemalizia ujumbe wake kwa kusema, “Tumuombee yeye na familia yake. Tusaidie kutoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwake.”

Godbless Lema, ambaye ni waziri kivuli wa Mambo ya Ndani aliandika katika Twitter, “Kama waziri kivuli wa Mambo ya Ndani, ninafuatilia kwa karibu suala la kutekwa mfanyabiashara Mo Dewji.”

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Kabwe aliandika, “Nimeshtushwa na kuumizwa na habari za kutekwa kwa ndugu yetu Dewji leo alfajiri akiwa anakwenda mazoezini hapa Dar es Salaam.”

“Kila mmoja wetu mwenye taarifa zozote zinazoweza kusaidia kumwokoa asaidiane na vyombo vyetu vya dola. Mola atamsaidia MO na familia yake katika mtihani huu.”

Bashe, Mbunge wa Nzega Mjini aliandika, “Inasikitisha na kushtua tukio hili la Dewji kutekwa. Aina hii ya uhalifu inaota mizizi, ana familia, ana watoto, ana ndugu tuendelee kumuombea kwa Allah na kila mmoja wetu kutoa taarifa yoyote atakayopata ambayo itasaidia kumpata akiwa salama Allah amlinde.”

Bashe aliweka picha ya Mo Dewji kisha akaandika ‘Oooh GOD’ na alama inayooshea kutoa machozi.

Mwanza, Kilimanjaro wazungumza

Baadhi ya wakazi jijini Mwanza wameiomba Serikali kuchukua hatua kukabiliana na matukio ya watu kutekwa au kupotea katika mazingira ya kutatanisha yanayoanza kushamiri nchini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na maeneo tofauti jana, wakazi hao walisema tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara huyo ni kama kutuma ujumbe kwa Serikali na vyombo vya dola kuwa hali ya usalama imetetereka na Tanzania inaanza kupoteza sifa ya kisiwa cha amani na utulivu iliyojijengea kwa muda mrefu.

“Ni dhahiri Tanzania usalama upo shakani, matukio ya watu kutekwa na kupotea yanaanza kuonekana kama ya kawaida. Ilianza kwa Ben Saanane, akafuata Azory Gwanda na leo ni kwa tajiri Mohammed Dewji. Hatujui atafuata nani kesho?” alisema Ahmed Chonza, mkazi wa Mtaa wa Kenyatta, Mwanza.

Mkazi wa Iloganzara, Said Ismail alisema Watanzania wanaanza kuingiwa na hofu juu ya usalama wao huku akisihi vyombo vya dola kuwasaka wahusika wa matukio ya utekaji bila shinikizo.

Wakati wengine wakihusisha tukio hilo na uhalifu wa kawaida, Getruda Wami, mkazi wa Luchelele alisema kutekwa kwa Dewji kunaweza kusababishwa na ushindani, ugomvi au dhuluma za kibiashara.

Mtu mwingine, Theophil Sued alisema licha ya kuwa tukio hilo ni la kihalifu, limetia doa sifa ya Tanzania na huenda ikatumiwa kufifisha juhudi za Serikali za kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nje ya nchi.

“Dewji ni mfanyabiashara na tajiri siyo tu nchini bali Afrika na dunia kwa ujumla, kitendo cha kutekwa kinatuma salamu na sifa mbaya nje ya nchi,” alisema Sued.

Kilimanjaro

Wananchi mkoani Kilimanjaro, wamekuwa na maoni tofauti kuhusiana na kutekwa kwa mfanyabiashara huyo, huku wengi wakisema kuwa tukio hilo limeibua hofu kwa wananchi.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Frederick Shoo alisema ni wakati wa Watanzania kumuomba Mungu ili kuwezesha kupatikana kwake akiwa mzima.

“Kutekwa kwa mfanyabiashara huyu ni jambo la kustusha na kubwa ni kuomba Mungu apatikane akiwa mzima, tunaomba pia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kufanya jitihada ili kuwezesha kupatikana kwake,” alisema Shoo.

Baraka Malya, ambaye ni mfanyabiashara mjini Moshi alisema tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara huyo ni la kusikitisha kwa kuwa nchi yetu inatambulika na kusifika kwa amani na utulivu.

Malya alisema tukio hilo linaibua hofu kwa wafanyabiashara na kuibua taswira mbaya kwa nchi kwa kuwa utamaduni wa utekaji haujazoeleka nchini.

“Huu si utamaduni mzuri kwetu, Serikali ifanye uchunguzi wa haraka kuwezesha kupatikana kwake akiwa mzima,lakini pia idhibiti matukio ya namna hii maana yanatutia hofu wafanyabiashara,” alisema Malya.

“Tumesikia ametekwa na raia wa kigeni, hili limetutia mashaka zaidi, suala kwa nini alikuwa peke yake si la kujadili kwa kuwa nchi yetu ni nchi ya amani na utulivu na ni kawaida kabisa kwa watu wakiwemo wafanyabiashara kutembea wenyewe bila walinzi,” alisema.

Profesa John Boshe alisema tukio la kutekwa kwa Dewji, mbali na kutia hofu, limeacha maswali mengi ambayo wananchi wakiyatafakari hawapati majibu yake.

Boshe, ambaye ni mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU) alisema kuna haja ya Serikali kwa kushirikiana na vyombo vyake vya ulinzi na usalama, kuongeza nguvu na kuhakikisha matukio ya namna hiyo yanakomeshwa nchini.

“Tunaomba Serikali iongeze nguvu Dewji apatikane akiwa salama, kwa sababu ni mtu maarufu na tukio hili limeshtua wengi, na ni vema wahusika wakipatikana, wachukuliwe hatua za kisheria kwa kuwa limeibua hofu kubwa kwa wananchi wa kawaida na hata walio maarufu nchini,” alisema Prpfesa Boshe.

Imeandikwa na Kelvin Matandiko, Tumaini Msowoya, Khatimu Naheka, Fortune Francis, Florah Temba na Hussein Issa