Mobetto, Ruby na Barnaba kupamba Miss Tanzania leo

Muktasari:

Wakati Mobetto akiwa mwongozaji wa shindano hilo, wasanii Ruby na Barnaba watatoa burudani katika shindano

 


Dar es Salaam. Saa chache kabla ya kuanza shindano la kumsaka mrembo wa Tanzania leo Jumamosi Septemba 8, 2018, mwanamitindo Hamisa Mobetto ametajwa kuwa miongoni mwa watakaopamba shindano hilo.

Hamisa na Deogratius  Kithama ndio watakaoongoza shindano hilo litakalofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC).

Jopo la majaji wa shindano hilo tayari limewekwa wazi na miongoni mwao ni mwanahabari mkongwe, Jenerali Ulimwengu.

Wengine ni waliowahi kushinda shindano hilo, Aina Maeda (1994) na Faraja Kota (2004), pia yupo mkurugenzi wa Bodi ya Utalii,  Devotha Mdachi na mtangazaji wa Clouds FM, Kennedy The Remedy huku wasanii Ruby na Barnaba wakitarajiwa kutoa burudani.

Warembo 20 watashuka jukwaani kuwania taji hilo la urembo na mshindi  ataiwakilisha nchi katika shindano ya Miss World litakalofanyika Desemba 8, 2018, Sanya nchini China.