Sunday, November 19, 2017

Mstaafu wa mafao ya Sh1.75 bilioni ajitokeza, ataka kumuona Magufuli

Mwalimu mstaafu alikuwa akifundisha shule ya

Mwalimu mstaafu alikuwa akifundisha shule ya Msingi Bwilingu B Halmashauri iliyopo Chalinze Mkoa wa Pwani, Mwachano Ramadhani akionyesha nyaraka za madai ya sehemu ya mafao yake juzi. Picha na Elias Msuya 

By Elias Msuya, Mwananchi emsuya@mwananchi.co.tz

Chalinze. Mwachano Ramadhani Msingwa, mmoja wa wastaafu waliotajwa na Rais John Magufuli kuwa wanadai mafao ya mabilioni ya fedha, amejitokeza akisema hayatambui.

Mwachano na wastaafu wengine wawili, walitajwa na Rais Novemba 6 wakati akizindua Uwanja wa Ndege wa Bukoba mkoani Kagera. Siku hiyo Rais alisema Sh159 bilioni zitatumika kulipa malimbikizo ya stahiki za watumishi wa umma.

Rais pia alisema watumishi watatu wameandika madai isivyo halali na kuwataja kuwa ni Jackson Kaswahili aliyesema anadai Sh7.62 bilioni, Mwachano Ramadhani (Sh1.75 bilioni) na Gideon Zakayo (104 milioni). Alisema baada ya uhakiki imebainika kiasi cha fedha wanachodai si sahihi.

Hata hivyo, Mwachano amekana kuandika madai hayo akisema anataka kuonana na Rais Magufuli amueleze ukweli kwa kuwa vielelezo vyote anavyo.

“Nataka nimuone Rais Magufuli nimweleze kilio changu. Mimi ni mwalimu na ni mama, siwezi kusema uongo na vielelezo vyote ninavyo,” alisema.

Mwachano, aliyekuwa mwalimu katika Shule ya Msingi ya Bwilingu “B” iliyopo Halmashauri ya Chalinze mkoani Pwani, alistaafu Januari 7 baada ya kuitumikia Serikali tangu mwaka 1984 na alishalipwa kiinua mgongo tangu Julai 30.

Mwalimu huyo ameshafundisha shule za msingi kadhaa, zikiwemo za Majengo, Lugoba, Kimange, Masuguru, Mwetemo na Bwilingu ‘B’.

Gazeti hili lilifika nyumbani kwake ambako bado anaishi kwenye nyumba ya Shule ya Msingi Bwilingu “B” na kumkuta mwalimu huyo mstaafu akiendelea na kazi zake za nyumbani.

Akizungumza na gazeti hili katika ofisi ya mwalimu mkuu wa shule hiyo, Mwachano alisema kabla ya kutajwa na Rais Magufuli, Oktoba 22 alipokea simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa anafanya kazi Hazina.

“Akaniuliza kama nina madai Serikalini,” alisema Mwanchano.

“Mtu huyo alisema amekwenda wilayani Bagamoyo kuulizia madai yangu akaambiwa niko Halmashauri ya Chalinze, hivyo kama nina barua za madai nizipeleke Hazina.”

Alisema kwa kumbukumbu zake yeye alikuwa akidai fedha za mizigo tu na hata alipokwenda kumuuliza mwalimu mkuu wa Bwilingu “B”, alimhakikishia hilo.

“Hata nilipokwenda kwa ofisa elimu aliniambia madai niliyobakiza ni nauli ya mizigo tu. Baada ya kukubaliana na mwalimu mkuu, nikaandika barua ya madai ya nauli ya mizigo. Mwalimu akanipigia muhuri, nikaenda ofisi ya kata nako nikapigiwa muhuri,” alisema.

Alisema baadaye aliipitisha kwa ofisa elimu wa Chalinze na kuipeleka barua yake Wizara ya Fedha Oktoba 23.

“Nilipofika Hazina, yule aliyenipigia simu sikumkuta. Sauti yake ni ya dada. Nikampigia simu akasema hakuwa kazini bali atampigia simu mtu hapo aje aichukue barua yangu.”

“Baada ya muda nikaona kuna mtu kama yeye ameshikilia simu. Akauliza kuna mwalimu Msingwa hapa? Nikamjibu ni mimi, akasema anahitaji barua yangu, nikampa nikarudi zangu nyumbani.”

Alisema baada ya siku hiyo, yule dada aliyempigia simu awali alisema ameipata ile barua na ameona katika jalada lake la ajira kuna fomu za kupandishwa daraja pia anatakiwa alipwe.

“Nikachukua barua ya tuzo ya PSPF, nikampa salary slip, barua za likizo zilizokuwa zimepigwa mihuri pamoja na barua ya kupandishwa daraja. Hiyo ndiyo iliyozua mambo kibao,” alisema Mwachano huku akichambua nyaraka zake.

Alisema yule dada alimwambia anapaswa kudai nyongeza ya mishahara ya kupandishwa daraja tangu Machi 2016.

“Oktoba 31 akanipigia simu akisema niende kwa mkurugenzi mtendaji wa Chalinze ili apate daraja langu la tangu Machi 2016. Nikarudi tena kwa mwalimu mkuu nikamweleza hayo yote,” alisema.

Mwachano alisema kuna wakati waliambiwa wajaze fomu za kupandishwa daraja na walimu wenzake ambao baadhi yao pia wameshastaafu na baada ya kujaza wenzake walipandishwa, lakini yeye hakupandishwa.

“Mwalimu mkuu aliposikia kuhusu madaraja hakushangaa, ikabidi niandike barua ya pili kama alivyonielekeza yule dada. Katika barua hiyo, Mwanchano aliomba malimbikizo ya mshahara baada ya kupandishwa daraja tangu Machi 2016.

Aliipeleka barua hiyo kwa ofisa elimu wa Chalinze na baadaye kwa ofisa utumishi na baada ya kupitishwa alitaka aipeleke Hazina, lakini muda ulikuwa umekwenda na hivyo kuamua kuipeleka siku iliyofuata.

“Ilikuwa saa moja jioni nikiwa nyumbani, kuna mwanangu yuko kijijini alinipigia simu akaniuliza, ‘Mama mbona umetajwa na Magufuli?” nikashangaa nimetajwa!” alisema.

“Nimelala asubuhi nikitarajia kesho yake niendelee kufuatilia madai yangu ya kupandishwa daraja. Kesho yake wakati najiandaa asubuhi nikamsikia tena Rais Magufuli akirudia hotuba yake na nikasikia akinitaja. Sijui nadai Sh1.75 bilioni, mimi nimezipata wapi?” Alihoji.

“Sikwenda tena Chalinze kuulizia barua yangu imekuwa vipi wala vipi.”

Alisema siku tatu baadaye walikuja watu waliojitambulisha kuwa maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa waliomhoji sambamba na mwalimu mkuu wa shule hiyo.

Mbali na maofisa hao, alisema ameshahojiwa pia na maofisa wa Takukuru na amewapa ushirikiano wa kutosha.

Mwachano alilionyesha gazeti hili malipo yake ya pensheni yanayoonyesha kuwa alilipwa Sh68.77 milioni na kwa sasa anapokea Sh369,711 kwa mwezi.

Mwalimu mkuu wa Bwilingu, Bibiana Thomas alisema kwamba anamfahamu Mwachano pamoja na sakata hilo.

-->