Mtaji wa Benki M wafikia Sh1 trilioni

Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo, Jacqueline Woiso

Muktasari:

Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo, Jacqueline Woiso alisema taasisi nyingine hutumia miaka 17 kukuza rasilimali hata mtaji wake kufikia kiwango hicho.

Dar es Salaam. Licha ya kuyumba kwa sekta ya fedha nchini, mtaji wa Benki M umeongezeka na kufika zaidi ya Sh1 trilioni ndani ya miaka 10 tangu ianzishwe.

Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo, Jacqueline Woiso alisema taasisi nyingine hutumia miaka 17 kukuza rasilimali hata mtaji wake kufikia kiwango hicho.

“Tumepata mafanikio makubwa ndani ya muda mfupi ambayo kila mtu anajionea. Tumeleta mapinduzi katika teknolojia ya kibenki, huduma kwa wateja, faida na kusaidia jamii,” alisema.

Tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, Novemba ya mwaka 2015 na kuagiza akaunti zote za taasisi za umma zihamishiwe Benki Kuu huku ikibana matumizi, sekta ya benki ni miongoni mwa zilizoathirika zaidi.

Uhakiki wa watumishi hewa ni suala jingine lililoziongezea mikopo isiyolipika lakini pamoja na hayo yote, Benk M inasema haikuyumba sana kwani miaka miwili tu baada ya kuanzishwa kwake, ilianza kupata faida.