Mtanzania akamatwa na dawa za kulevya India

Muktasari:

Gazeti la kila siku nchini humo la New Delhi limesema mtuhumiwa huyo alikamatwa Jumanne wiki hii kwenye Uwanja wa Ndege wa Indira Ghandhi jijini Delhi.

Dar es Salaam. Kitengo cha dawa za kulevya nchini India (NCB), kimemkamata Mtanzania, Brayton Lyimo (31) akiwa na dawa aina ya heroine.

Gazeti la kila siku nchini humo la New Delhi limesema mtuhumiwa huyo alikamatwa Jumanne wiki hii kwenye Uwanja wa Ndege wa Indira Ghandhi jijini Delhi.

Taarifa hiyo imesema kwamba Mtanzania huyo alikamatwa baada ya kushuka uwanjani hapo akiwa na dawa hizo zenye thamani ya Dola 160,000 za Marekani ambazo ni takribani Sh400 milioni.

Mtanzania huyo ambaye sasa anashikiliwa na taasisi hiyo alikuwa akitokea Mumbai.

“Mtuhumiwa alihojiwa na maofisa wa kitengo cha dawa za kulevya baada ya kutiliwa shaka ikiwa ni jitihada za kuzuia genge la kimataifa la biashara ya dawa za kulevya,” imeeleza taarifa hiyo.

Maofisa wa taasisi hiyo wanasema Lyimo alikuwa ameshika vifurushi viwili vya heroine vyenye kilo 4.8 ambavyo viliwasili Mumbai kutoka Addis Ababa (Ethiopia).

Taarifa ya maofisa hao inaonyesha kwamba, baada ya kushuka uwanja wa Mumbai, mtuhumiwa huyo alipanda ndege kuelekea New Delhi ambako walifanikiwa kumkamata.

Imebainishwa kwamba dawa alizokamatwa nazo Lyimo zilitokea nchini Tanzania ambazo alitakiwa kuziwasilisha kwa raia wa Nigeria aishie New Delhi.

Imeelezwa pia kuwa, Mtanzania huyo alishafanya safari nyingine ya kwenda India Januari mwaka jana.

Mkurugenzi  wa kitengo cha dawa za kulevya India,  Madho Singh amesema wanaendelea na uchunguzi zaidi, huku wakichunguza mawasiliano aliyofanya sehemu mbalimbali.