Mtanzania jela miaka 5 Ghana kwa ‘unga’

Muktasari:

Taarifa kutoka Accra nchini Ghana, zinasema Mtanzania huyo alihukumiwa baada ya kukiri kosa la kusafirisha dawa hizo.

Matukio ya Watanzania kukamatwa na dawa za kulevya yameendelea kutawala, baada ya Basaida Zena Jafary kuhukumiwa miaka mitano nchini Ghana baada ya kupatikana na gramu 300 za dawa za kulevya.

Taarifa kutoka Accra nchini Ghana, zinasema Mtanzania huyo alihukumiwa baada ya kukiri kosa la kusafirisha dawa hizo.

Mtanzania huyo alikamatwa na maofisa wa bodi ya kupambana na dawa za kulevya nchini Ghana (Nacob), kwenye Uwanja wa Ndege wa Ndege wa Kimataifa wa Kotoka (Kia) wiki mbili zilizopita akiwa na kilo mbili na gramu 300 za Heroine na Cocaine.

Taarifa zilizotolewa na bodi hiyo na kunukuliwa na redio ya Star FM Online ya mjini Accra, zinasema dawa hizo zilikuwa na thamani ya dola 70,000 (Sh170 milioni) na kwamba, alikuwa akiwasili nchini humo na ndege ya shirika la ndege la Rwanda yenye namba ET 200.

Taarifa hizo zinasema baada ya kukamatwa, alifanyiwa upekuzi kwenye mzigo ikabainika alikuwa amebeba dawa za kulevya.

Baada ya kugundilika kuwa ni dawa za kulevya, maofisa wa bodi hiyo walimpeleka kwenye mamlaka ya viwango kwa ajili ya uthibitisho ambayo pia ilibaini kwamba mzigo ule ulikuwa ni dawa.

Alipohojiwa alithibitisha kuwa ndiye mmiliki wa mzigo huo na alipewa na mtu mmoja ambaye alimtaja aishie Tanzania, ambaye alimuagiza kuufikisha nchini Ghana kwa malipo ambayo hayakufahamika.