Mtei: Hamahama itaupa upinzani dola 2020

Edwin Mtei


Muktasari:

Ushiriki wa wabunge wa upinzani ndani ya Bunge unaonekana kuendelea kuwa finyu kutokana na hamahama, huku halmashauri zikizidi kupoteza idadi kubwa ya madiwani na wenyeviti walioingia madarakani kwa wingi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Kama kuna wakati vyama vya siasa vimewahi kukumbwa na msukosuko mkubwa, basi ni kipindi hiki ambacho wabunge na madiwani wanatangaza kuhama usiku na mchana kurejea chama tawala cha CCM.

Ushiriki wa wabunge wa upinzani ndani ya Bunge unaonekana kuendelea kuwa finyu kutokana na hamahama hiyo, huku halmashauri zikizidi kupoteza idadi kubwa ya madiwani na wenyeviti walioingia madarakani kwa wingi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Wengi wanaona hizi si dalili nzuri kwa siasa za Tanzania, hasa mustakabali wa vyama vya upinzani ambavyo hakuna shaka vimekuwa na mchango katika maendeleo ya Taifa tangu siasa za ushindani ziliporejeshwa mwaka 1992.

Lakini, mmoja wa wasisi wa Chadema, Edwin Mtei si miongoni mwa watu wenye hofu hiyo ya upinzani kutoweka; yeye anaona hamahama hiyo kuwa yaweza kuifanya Chadema kuchukua nchi mwaka 2020.

Mtei alisema hayo katika mahojiano na Mwananchi yaliyofanyika nyumbani kwake Tengeru wilayani Arumeru kuhusu mwenendo wa wabunge wa upinzani kukimbilia CCM na kupewa nafasi ya kutetea nafasi walizojiuzulu.

“Matukio hayo ndio yanaendelea kuimarisha upinzani na hivyo wanaohama waachwe wahame,” alisema Mtei, ambaye alikuwa na mchango kuhakikisha nchi haiyumbi kiuchumi akiwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Hadi jana wabunge saba na zaidi ya madiwani 50 wa Chadema wamejivua uanachama na kujiunga na CCM. Wabunge waliojiuzulu ni Julius Kalanga (Monduli), Mwita Waitara(Ukonga), James Millya (Simanjiro), Paulina Gekul (Babati Mjini), Marwa Ryoba (Serengeti), Dk Godwin Mollel (Siha) na Joseph Mkundi (Ukerewe).

“Wabunge wanaohama sasa wanajali maslahi yao. Waache waende, mimi bado nina imani Uchaguzi Mkuu ujao 2020 upinzani unaweza kushika dola,” alisema.

Alisema ingawa vitendo vya kuondoka wabunge vinasababisha hasara kubwa kwa Taifa, suala hilo haliwezi kuzuiwa na upinzani kwa kuwa wanaohama wanajua wanachokifuata CCM .

“Hoja ya gharama kubwa ni sawa, lakini wengine wanataka kutatua migogoro yao ya kisiasa kutokana na kutokubaliana na misimamo ya viongozi wao,” alisema.

Mtei alisema bado ana imani kuwa Chadema itaendelea kupokea wanachama wapya wenye malengo yanayofanana katika kutetea demokrasia na maendeleo.

Pia, alizungumzia hoja ya uenyekiti wa Freeman Mbowe ambayo imetajwa na baadhi ya wabunge wanaohama kuwa moja ya sababu ya kuhama kwao.

Hoja hiyo pia imekuwa ikitajwa na baadhi ya wanasiasa wa CCM, wakidai kuwa mbunge huyo wa Hai amekaa madarakani muda mrefu na hivyo Chadema inahitaji kiongozi mpya mwenye maono tofauti.

Lakini, Mtei haungani na upande wowote wa sauti hizo, bali anajikita katika hoja ya misingi ya uongozi na uzoefu wake katika kupokezana vijiti akiwa mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Mtei (86) anasema Mbowe si mwenyekiti wa maisha wa chama hicho na kwamba wakati ukifika atampisha mwingine.

“Mbowe hategemei kuwa atakuwa hapo (nafasi ya uenyekiti) maisha,” alisema Mtei aliyejiunga na siasa za upinzani kwa kuanzisha chama hicho mwanzoni mwa miaka ya tisini.

“Itategemea Katiba (ya chama) na afya yake. Hakuna mtu ambaye tunafikiri atakuwa ni wa kudumu katika uongozi wa chama chetu.”

Mbowe, ambaye amekuwa mwenyekiti wa Chadema tangu mwaka 2004, anasifika kwa kuifanya Chadema kuwa chama kikuu cha upinzani kikiviacha nyuma vyama vingine vilivyotikisa nchi mwanzoni mwa siasa hizo za ushindi, hasa NCCR-Mageuna CUF.

Mmoja wa watu wanaodai Mbowe anatakiwa aondoke ni Mwita Waitara, ambaye aliitisha mkutano na waandishi wa habari kueleza msimamo wake dhidi ya uenyekiti wa Mbowe, akidai ni moja ya sababu za kujivua uanachama na kujiunga CCM.

Lakini mara zote Chadema imesimama imara na kusema bado Mbowe ni mwenyekiti anayefaa kuliongoza kundi hilo kwa sasa.

Mtei alisema Katiba ya Chadema haijasema kutakuwa na mwenyekiti wa maisha kama baadhi ya watu wanavyotaka kupotosha.

Alisema anategemea muda ukifika, Mbowe ataondoka Chadema na kumpisha mwanachama mwingine mwenye sifa na uwezo kwa mujibu wa katiba.

“Mbowe hafanyi mambo yake kisiri, ni kiongozi wa upinzani bungeni. Kama ikitokea tofauti, kwa kushirikiana na viongozi wenzake wanachukuwa hatua. Sisi tunaendelea kumsupport (kumuunga mkono) na anajua chama kipo nyuma yake,” alisema mwanasiasa huyo mkongwe.

Mtei alisema yeye kama muasisi wa Chadema anaona Mbowe pamoja na wengine wanaendelea kukiongoza chama hicho vizuri kama katiba inavyoelekeza.

“Haya yanayotokea sasa ndio ukomavu wa demokrasia. Wanachama waendelee kupewa fursa na uhuru wa kuzungumza. Na kutofautiana mawazo ni mambo ya kawaida,” alisema.